Mgombea atiwa mbaroni tuhuma za kudanganya kutekwa

By Remmy Moka , Nipashe
Published at 03:28 PM Nov 29 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikiria Aliyekuwa Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Buswelu A kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Apolinali Shule kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema walipata taarifa 26/11/2024 majira ya mchana katika vyombo vya habari  kuhusu taarifa ya Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje  akielezea kutoweka kwa mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa mtaa wa Buswelu A Pastori Apolinali Shule 51.

Kamanda amesema Wenje alisema mgombea huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha na ametekwa na maisha yake yapo hatarini na kuliomba Jeshi la Polisi kumtafuta mgombea huyo kwa usalama zaidi

Ameongeza kuwa mara baada ya taarifa hiyo Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi  ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo  kwa lengo la kuokoa maisha ya mgombea huyo.

Ameongeza kuwa walimuhoji mke wa mgombea huyo Maria Mchonyo na  Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Buswelu A, Godson Mkama ambaye alisema taarifa hiyo haikuwa na ukweli wowote kwani alikutana na mgombea huyo na kumueleza kwamba hapendi kuendelea na mchakato wa kinyang'anyiro cha uchaguzi wa serikali za mitaa.