CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kimeibuka na ushindi wa asilimia 99.7 katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa kuwachagua wenyeviti wa vijiji, mitaa, vitongoji na wajumbe.
Katibu Mwenezi wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Singida, Elphas Lwanji akizungumza na waandishi wa habari leo (Novemba 29,2024) amesema ushindi huo wa CCM umetokana na imani kubwa waliyonayo wananchi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameleta maendeleo makubwa nchini.
Lwanji amesema katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba 27, 2024, CCM imeshinda mitaa yote 53 Vijiji vyote 441 vilivyopo katika Mkoa wa Singida sawa na ushindi wa asilimia 100.
Amesema kati ya vitongoji 2289 vilivyopo mkoani hapa, CCM imepata ushindi katika vitongoji 2,279 sawa na ushindi wa asilimia 99.7 ambapo vyama vya upinzani vimepata vitongoji 8 na vitongoji viwili havikufanya uchaguzi kutokana na sababu zilizoelezwa na Waziri Ofisi Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa.
Lwanji ameongeza kuwa katika nafasi ya wajumbe viti maalum na wajumbe mchanganyiko CCM imeibuka na ushindi wa asilimia 100.
“CCM mkoa Singida tunawashukru wananchi kwa jinsi walivyoweza kuonyesha imani kwa chama na kwa rais na hivyo tuna imani changuzi zijazo wataendelea kuwa na imani kwa rais, chama na serikali yao na hakika tutapata ushindi wakati wote,”alisema.
Aidha, amewataka waliochaguliwa kutekeleza majukumu yao kama ilani ya CCM inavyoelekeza na kwamba chama kitaendelea kuwasimamia kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya wananchi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED