Msongamano wa Malori wageuka tishio mtaa wa Saza Road Chang’ombe Dar

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 08:29 PM Nov 29 2024
Msongamano.

MSONGAMANO wa malori kwenye mtaa wa Saza Road Kata ya Changombe jijini Dar es Salaam umegeuka kuwa kero kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Malori hayo ambayo yamekuwa yakiegeshwa barabarani yamekuwa yakifunga barabara muda mwingi na kusababisha watumiaji wa barabara kupita kwa shida.

Mmoja wa watumiaji wa barabara hiyo, Amir John aliomba Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) kufika eneo hilo kuona hali halisi kwanai ni hatari iwapo janga la moto litatokea.

“Njia ya Saza Road na Mwakalinga muda wote malori yameegeshwa barabarani tunapita kwa shida sana na tunajiuliza iwapo itatokea dharura ya moto magari ya zimamoto yatapita wapi, TARURA, Polisi Temeke  waje waone na kutatua kero hii,” alisema

“Wakati wa mchana na jioni hali inakuwa mbaya sana malori yameegeshwa barabarani jambo ambalo halitakiwi tunaomba TARURA waje waone,” alisema mtumiaji mwingine wa barabara hiyo John Mwakitwange.

Gazeti hili lilimtafuta Ofisa wa TARURA aliyefahamika kwa jina la Allan Mamkwe, ambaye aliahidi kuwa wataifanyia kazi changamoto hiyo.

“Nakuahidi kwamba  tumeichukua hiyo changamoto na tutalifanyia kazi,” alisema Allan

Polisi wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam mchana walionekana wakihangaika kutatua kero hiyo kwa kubandua namba za magari yaliyoegeshwa katikati ya barabara.

Baadhi ya madereva wamemlaumu mkandarasi anayejenga kipande cha barabara ambacho kwa sasa kimefungwa na kusababisha kero hiyo.