SERIKALI imesema itatumia mfumo wa ushirikiano na sekta binafsi (PPP) katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (BRT) na mwezi ujao watoa huduma watatu wataleta mabasi yao ili kuondoa tatizo la usafiri lililopo hivi sasa.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema Dar es Salaam ina tatizo la mabasi ya mwendokasi na serikali imeshafanya uamuzi -- inatumia sekta binafsi kuongeza mabasi katika mradi huo.
"Tunatarajia mwezi wa tatu (Machi) watoa huduma wataanza kuleta hayo mabasi, tumepata watoa huduma watatu kwenye ile barabara mpya ya kwenda Mbagala, huko kuna maswali mengi sana. Watoa huduma wataleta mabasi mengi na ya kutosha lakini pia UDART (Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka) nao wanaongeza mabasi 150.
"Tunaamini haya yote yakiingia huko na wakati serikali inaendelea kufanya kazi na sekta binafsi, tunaamini msongamano kwa Jiji la Dar es Salaam utapungua kwa kiasi kikubwa na uwekezaji mkubwa unaoendelea Dar es Salaam wa barabara zile na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka yanafungua maeneo mengi," alisema.
Kuhusu mvutano wa mabasi kutofika Kibaha, Msigwa alisema serikali inalifahamu na inalifanyia kazi. Muda si mrefu yataendelea kutoa huduma.
Alisema kila taasisi iliyopangwa kwa ajili ya kuzungumzia mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni lazima ifike kwenye Idara ya Habari Maelezo kuzungumza na ambazo hazitafika zitapaswa kujieleza.
Msigwa alisema kuwa hivi sasa zimeanza taasisi za serikali hadi Februari 27 na baada ya hapo, Machi 14 wataanza mawaziri kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio hayo.
Awali, Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Ephatar Mlavi, alisema awamu ya tatu ya ujenzi wa BRT inahusisha urefu wa Km 23.3 katikati ya Jiji hadi Gongo la Mboto.
Alisema ujenzi huo umefikia asilimia 74, awamu ya nne ya Km 30.1 kutoka katikati ya Jiji hadi Tegeta ambao umefikia asilimia 22 huku awamu ya tano kutoka Ubungo – Bandarini na Segerea – Tabata – Kigogo, Km 25.4 uko katika hatua za mwisho za ununuzi.
Hivi karibuni, katika mkutano wa 18 wa Bunge, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilibaini kuwapo tija ndogo kwenye uendeshaji wa mradi huo huku barabara ya Kimara – Kivukoni, ikiwa na mabasi 100 yanayofanya kazi badala ya 305.
Kufuatia hali hiyo, kamati ilielekeza DART iharakishe kupata watoa huduma kwa awamu zote tatu ili mradi huo uendeshwe kwa ukamilifu wake, ili tija ya uwekezaji wa mtaji wa umma ipatikane.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Vuma, alisema kamati ilichambua taarifa za utekelelezaji mradi huo na kubaini kuwa tija na ufanisi ni ndogo ambapo serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika awamu tatu ambapo jumla ya Sh. bilioni 847.03 kwa awamu ya kwanza na ya pili zimetumika na Dola za Marekani milioni 148.2 kwa awamu ya tatu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED