Mpigapicha, mwandishi Nipashe wakamatwa Dar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:36 PM Sep 23 2024
Mpigapicha, mwandishi Nipashe wakamatwa Dar

MWANDISHI wa Habari na Mpigapicha wa Gazeti la Nipashe, wamekamatwa na polisi wakati wakitimiza majukumu yao ya uandishi wa habari kwenye eneo la Buguruni na Ilala ambako viongozi na wanachama wa CHADEMA walikuwa wakiandamana.

Mpigapicha Jumanne Juma alikamatwa eneo la Kituo cha Mafuta Buguruni wakati akipiga picha wanachama wa CHADEMA waliokusanyika eneo hilo kwa ajili ya kutekeleza maandamano yao.

Baada ya kukamatwa alipelekwa Kituo cha Polisi Buguruni, ambako alihojiwa kwa saa moja kadhaa akiulizwa kwanini wanapiga picha wakati hakuna maandamano.

“Nilivyofika nilikwenda kujitambulisha kwa kiongozi wa Askari waliokuwepo lakini baada ya muda walituzunguka wakatukamata mimi na mwandishi wa mwananchi, tukapelekwa kituoni tukahojiwa, baadaye wakatupeleka kwa Mkuu wa Kituo ambaye aliwaambia kama mmewahoji na hawana madhara waachieni, ndipo tunaaachiwa,”amesema Jumanne.

Aidha, Mwandishi wa Nipashe, Jenipher Gilla amekamatwa wakati akikusanya taarifa za maandamano hayo kisha kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Akizungumza akiwa kituoni humo amesema alifikishwa kituoni humo kisha kuhojiwa kwanini alikuwa anakusanya taarifa kwenye eneo hilo.