ACT Wazalendo waiangukia CHADEMA

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:24 AM Sep 23 2024
ACT Wazalendo waiangukia CHADEMA
Picha:Nipashe Digital
ACT Wazalendo waiangukia CHADEMA

CHAMA cha ACT Wazalendo kimekiomba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kusitisha maandamano ya amani yaliyopangwa kufanywa leo, kikizitaka pande zote kurudi nyuma na kuwa na mazungumzo zaidi.

Kukiwa na rai hiyo ya ACT, mitaani jana askari wa Jeshi la Polisi walitanda kuimarisha hali ya ulinzi na usalama mkoani Dar es Salaam, hali hiyo ikishuhudiwa pia katika mikoa ya Morogoro na Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya.

CHADEMA imeshikilia msimamo wa kuendelea kuandamana kwa amani kuomboleza wenzao waliouawa na kushinikiza serikali kuchukua hatua kudhibiti mauaji na watu kutekwa.

Maandamano hayo yanalenga kuomboleza vifo vya viongozi wa chama hicho na matukio ya kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa wananchi yaliyoripotiwa nchini hivi karibuni.

Pia yanalenga kuishinikiza serikali kufanyia kazi maagizo waliyoipa Septemba 11, mwaka huu, ikiwamo kuwataka Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi kujiuzulu.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, ameomba CHADEMA kuahirisha maandamano ya amani na badala yake serikali ichukue hatua ili kujenga nchi.

Dorothy alisema jana kuwa mvutano huo umepelekea kila upande unaohusika kukaza kamba na kutetea msimamo wake, hali ambayo aliitaja "haitoi nafasi ya vichwa kutulia na kutafuta suluhisho la kiuongozi litakalotutoa hapa".

"Tunatoa wito pande zote kutuliza vichwa na kutoa nafasi kwa hekima na busara za uongozi zitumike kufanya ufumbuzi na suluhisho mwafaka.

"Tanzania inayo hazina ya watu wenye busara na hekima wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wetu wa dini ambao wakifanya kazi pamoja, wanaweza kututoa kwenye hali iliyopo sasa na tukatoka tukiwa imara zaidi kama taifa na hata kuwa mfano kwa wengine kama ilivyo historia yetu adhimu.

"Mimi binafsi (Dorothy Semu) na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Othman Masoud Othman tunafanya mazungumzo na pande zote mbili katika jitihada za kupata mwafaka wa hali tuliyo nayo," alisema Semu.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kupitia Twitter Space ya chama hicho jana, aliwakumbusha wananchi kuwa maandamano hayo yatafanyika leo kuanzia saa tatu asubuhi.

Alisema kuwa Septemba 11 mwaka huu, chama hicho kiliwataarifu Watanzania kuwa kitafanya maandamano hayo leo kama serikali haitoonesha mwanga wa kushughulikia maagizo walioyatoa kwayo, ikiwa ni sehemu ya kutafuta wanachokiita "suluhu ya matukio ya utekaji, utesaji, ya mauaji ya Watanzania wasio na hatia".

Alisema ndani ya miezi mitatu, viongozi sita wa chama hicho walitekwa katika mazingira yanayoashiria kuhusika kwa vyombo vya ulinzi na kuzua taharuki kwa wananchi.

Mbowe alisema taharuki iliongezeka baada ya kutekwa kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho taifa, Ally Kibao, Septemba 7 mwaka huu kisha kuuawa na mwili wake kukutwa ukiwa umetupwa eneo la Ununio, Tegeta, Dar es Salaam Septemba 8 mwaka huu, ukiwa na majeraha.

Alisema baada ya tukio hilo chama hicho kilizungumza na vyombo vya habari na kuwataka Waziri wa Mambo ya Ndani, Masauni na viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi kama sehemu muhimu ya uwajibikaji.

Mbowe alisema pia waliagiza kurejeshwa viongozi wao waliotekwa kwa zaidi ya mwezi mmoja, wakiwa hai au wamefariki dunia, wakiwamo Katibu Mwenezi wa Sumbawanga Mjini, Dionise Kipanya, Katibu wa Chama Wilaya ya Temeke, Jacob Mlay na Katibu Mwenezi, Muheza mkoani Tanga, Mbwana Kombo.

Alisema pia waliitaka serikali kuruhusu uchunguzi huru utakaofanywa na wachunguzi huru kutoka Scotland Yard kwa madai kuwa vyombo vya usalama nchini ni sehemu ya watuhumiwa wa matukio hayo, hivyo haviwezi kujichunguza.

Alisema kufuatia vitendo hivyo, chama hicho kilikubaliana kutangaza mwezi wa maombolezo, bendera zao zikipepea nusu mlingoti huku wakisubiri hadi Septemba 21, kama hakutokuwa na hatua zozote za kutoa mwanga kutoka serikalini, watafanya maandamano ya maombolezo jijini Dar es Salaam leo.

Alisema kuwa hadi Septemba 21, hakuna agizo lolote walilolitoa lililopewa nafasi ya kufanyiwa kazi na serikali au kujibiwa badala yake, wameona idadi kubwa wa askari wenye silaha kali wakiletwa Dar es Salaam wakiwa na silaha na magari ya aina mbalimbali, yakiwamo yenye maji ya kuwasha, farasi, mbwa, mabomu.

Mbowe alisema kwa mujibu wa sheria, waliiandikia barua polisi kuwaleza nia ya kufanya maandamano ya amani na maombolezo leo, lakini walitoa katazo badala ya ulinzi huku viongozi wao wakiendelea kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Mboye aliwasisitiza Watanzania kuwa maandamano hayo ni ya maombolezo na amani yasiyolenga kupambana na mtu yeyote wala kubeba silaha ya aina yoyote kwa lengo la kudhuru au kujeruhi mtu yeyote.

"Hatufurahii uvunjifu wowote wa sheria wala hatukusudii kuharibu amani ya nchi yetu kama inavyojaribu kuaminishwa na viongozi wa serikali," alisema Mbowe.

Alisema kuwa chama hicho kinafanya kazi zake kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi na kipo kwa mujibu wa Katiba ya nchi inayotoa haki ya kukusanyika na kujumuika.

Mbowe alirejelea pia Kifungu cha 11 (4) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, kinatoa haki ya chama kufanya maandamano kwa kutoa taarifa kwa OCD, jambo ambalo walifanya.

Alisema ni matumaini ya chama hicho kuwa serikali na vyombo vyake vyote vitaheshimu haki yao ya kikatiba na sheria na kulinda maandamano yao ya amani na maombolezo badala ya kuyazuia na kuyatawanya kwa nguvu.

"Hatutegemei falsafa ya maridhiano igeuke kuwa mafarakano, falsafa ya ustahamilivu igeuzwe hasira na chuki, falsafa ya mageuzi igeuzwe ukiritimba wa chama kimoja na ujenzi mpya ugeuzwe uadui na umwagaji damu," alisema Mbowe.

Kaimu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Tundu Lissu, alisema maandamano hayo si uhalifu na mara zote alizokuwa anakamatwa, hajawahi kutiwa hatiani.

Alisema amepata taarifa kuwa atakamatwa muda wowote kuanzia jana na kuwa amejiandaa kwa lolote na kuwa itakuwa ni mara ya pili kukamatwa na Jeshi la Polisi ndani ya miezi miwili, na mara ya 10 kukamatwa na Jeshi la Polisi ndani ya miaka minane, lakini alipona baada ya kupigwa risasi 16.

"Wakati wa uongozi wa (Benjamin) Mkapa nilikamatwa mara moja, wa (Jakaya) Kikwete mara tatu, wa (Dk. John) Magufuli mara nane. Hii itakuwa mara ya pili katika uongozi wa (Rais) Samia. Mara zote sijawahi kutiwa hatiani na mahakama yoyote, sijawahi kutenda kosa la jinai, mimi ni mpigania uhuru na haki", alidai.

Jana waandishi wa Nipashe walitembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kukuta askari polisi wakiwa na magari yenye maji ya kuwasha. Baadhi ya maeneo hayo ni Kituo Kidogo cha Polisi Kitunda, eneo la JET karibu na uwanja wa ndege, Taraza katika Daraja la Mfugale, Buguruni, Shekilango na Mwenge.

Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya jana zaidi ya magari 10 yenye askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Kikosi cha Mbwa na maji ya kuwasha yalionekana yakifanya doria kwenye mitaa mbalimbali.

Vilevile, mkoani Morogoro, askari polisi walionekana kwenye mitaa mbalimbali wakifanya mazoezi ya kawaida ya utayari.

Katika Mkoa wa Kipolisi wa Tarime Rorya, askari hao wakiwa kwenye magari, walionekana majira ya asubuhi, wakizunguka katika wilaya zote sita za Sirari, mjini Tarime, Nyamwaga, Utegi Shirati na Kinesi.

Alipoulizwa kuhusu misafara hiyo, Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, SACP Michael Njera, alisema hatua hiyo ni utaratibu wa jeshi hilo kuzungukia wilaya zao za kipolisi wakihimiza amani.

"Tunahimiza amani kwa taifa letu na kujiweka katika utayari kwa lolote linaloweza kutokea la uvunjivu wa amani. Tunawaasa wananchi kuwa na uzalendo na kutunza amani," alisema Kamanda Njera.

Pia aliwataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo katika kuimarisha ulinzi wa taifa kwa kutoa taarifa za viashiria vya uvunjivu wa amani na uhalifu kwa kuwa ulinzi na amani kuwapo kunahitaji ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi.

Mkoani Morogoro, Kamanda wa Polisi Alex Mkama alisema mazoezi yanayofanyika ni ya utayari kwa kutumia magari, kutembea na kukimbia.

"Mazoezi hayo yamefanyika leo (jana) kupita maeneo ya FFU, Kichangani, Msamvu, Kihonda, Mazimbu, Madeko, Chamwino, Tumbaku, Mafiga, Kiwanja cha Ndege, Maskika, Sabasaba, Boma Road na stendi ya zamani," alisema.

Alisisitiza kuwa mazoezi hayo ni ya kawaida na hufanywa na askari kila mwisho wa wiki kwa ajili ya kujiweka sawa.

Septemba 13, mwaka huu, Jeshi la Polisi lilipiga marufuku kufanyika maandamano hayo ya CHADEMA, likitoa sababu kuwa ni kielelezo cha uvunjifu wa amani.

Akiwa mkoani Arusha siku hiyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, alisema maandamano hayo ni haramu na kutoa onyo kwa viongozi wa CHADEMA kuacha kuendelea kuwahamasisha wananchi kujihusisha kwa kuwa ni uhalifu.

"Jeshi la Polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa, kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo, asithubutu kufanya hivyo kwani maandamano hayo ni haramu na hayatafanyika," alionya DCP Misime.

*Imeandaliwa na Samsoni Chacha (TARIME), Halfani Chusi na Jenifer Gilla (DAR)