Watendaji maabara uchunguzi wa sayansi jinai wapewa angalizo

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 11:18 AM Sep 23 2024
Watendaji maabara uchunguzi wa sayansi jinai wapewa angalizo
Picha: Mtandao
Watendaji maabara uchunguzi wa sayansi jinai wapewa angalizo

NAIBU Kamishna wa Polisi, Mwamini Rwantale, amewataka watendaji wa Jeshi la Polisi katika maabara za uchunguzi wa sayansi jinai kuzingatia weledi na maadili wakati wa utekelezaji shughuli zao ili kuepuka majibu yao kutiliwa shaka.

Kamishna Mwamini ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sayansi Asilia ndani ya jeshi hilo, alisema mwishoni mwa wiki kuwa majibu na vielelezo vya wataalamu hao kuhusu makosa ya jinai vinategemewa kutenda haki kwa jamii na vyombo vya uamuzi, ikiwamo mahakama katika kufanya uamuzi wa kisheria.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Uchunguzi wa Kisayansi wa Makosa ya Jinai (Forensic Day) ambayo kwa Tanzania ni mara ya kwanza kuadhimishwa, alisema itakuwa aibu majibu ya wataalamu kutoka maabara ya uchunguzi wa sayansi jinai yakitiliwa shaka na kufanyiwa uchunguzi tena ili kujiridhisha.

Alisema ni muhimu kwa wataalamu wa tasnia hiyo kuzingatia maadili kwa kuwa Jeshi la Polisi liko katika awamu ya pili ya maboresho ya utendaji kazi na utekelezaji mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

"Sayansi imekuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya binadamu katika kusaidia haki kutendeka, kwani kupitia uchunguzi wa sayansi jinai tumeshuhudia wahalifu wakibainika kirahisi, na kuunganishwa na tuhuma zinazowakabili pasipo shaka, huku wasio na hatia wakiachiwa huru.

"Mnaweza kuona ni kwa kiasi gani pale dunia itakapokuwapo pasipo ukweli, tutashuhudia wahalifu wakiachiwa huru, na wasio na hatia wakifungwa gerezani. 

"Hivyo, tunaadhimisha siku hii muhimu kama sehemu ya mapinduzi ya sayansi kwenye mchakato mzima wa utoaji haki," alisema Kamishna Mwamini.

Alieleza kuwa siku hiyo inaashiria kuwatambua mashujaa na wagunduzi wa uchunguzi wa kisayansi waliofanya kazi kubwa katika kuhakikisha sayansi inakwenda kutoa mchango wake kwenye mchakato mzima wa utoaji haki. 

Alisisitiza kuwa bila jitihada hizo, upatikanaji haki duniani ungeendelea kubaki kuwa ndoto. Pia alisema linapokuja suala la utafutaji haki, kila kitu kwenye eneo la tukio kina umuhimu mbele ya sayansi, akisema unywele mmoja, tone la damu, mwandiko kwenye karatasi na mambo mengine yanayohusiana, vyote ni muhimu katika kubaini ukweli.

Naibu Kamishna huyo alisema tasnia hiyo ni muhimu katika dunia ya leo hasa katika kubainisha ukweli na kusaidia haki kutendeka katika jamii.

"Sisi kama wadau wa uchunguzi wa sayansi ndani ya Jeshi la Polisi tunaamini katika kusherehekea siku hii inaonesha umuhimu wetu katika jamii, na imekuja kipindi mwafaka cha kuboresha utendaji wetu, ikiwamo kubadilika kifikra, kutenda kwa weledi na kuacha utendaji wa mazoea," alisema Kamishna Mwamini.

Mwakilishi kutoka Maabara ya Sayansi Jinai Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Fidelis Segumba, alisema katika utendaji wa shughuli zao, wanashirikiana na Jeshi la Polisi, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wataalamu wa eneo hilo kuzingatia weledi tangu wanapoanza kuchukua sampuli, kuzitenganisha vizuri hadi wanakozifikisha ili kuondoa mkanganyiko.