Majaliwa atinga UN, ateta na Katibu Mkuu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:38 AM Sep 23 2024
Majaliwa atinga UN, ateta na Katibu Mkuu
Picha: Mtandao
Majaliwa atinga UN, ateta na Katibu Mkuu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutierres katika makao makuu ya umoja huo na kujadiliana masuala kadhaa, yakiwamo ya maendeleo ya jamii, ulinzi na usalama, siasa na ushirikiano wa Tanzania na UN.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wao uliofanyika mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu ambaye yuko Marekani akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79), alisema kuwa katika suala la maendeleo ya jamii, wamejadiliana umuhimu wa kuinua uwezo wa wananchi kiuchumi, ikiwamo upatikanaji huduma zote muhimu.

Kuhusu ulinzi na usalama, Waziri Mkuu alisema Tanzania imepongezwa kwa kusimamia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, hasa za ukanda wa Jumuiya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

"Sasa hivi serikali yetu inaendelea kuunga mkono kwa kupeleka vikosi vya ulinzi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na za SADC," alisema.

Majaliwa aliongeza: "Katika hili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amempongeza sana Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, wananchi na serikali kwa ujumla katika kuhakikisha Bara la Afrika linabaki kuwa salama."

 Kuhusu siasa, Waziri Mkuu alimweleza Katibu Mkuu huyo kuhusu kuwapo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba, mwaka huu na Uchaguzi Mkuu ujao na kusisitiza haja ya kila mtu kushiriki uchaguzi huo na haki ya kuchaguliwa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu amepongeza Tanzania kwa jinsi ilivyoshiriki kusaidia Burundi kuwa salama kwa kuendelea kuwapokea wakimbizi katika kipindi chote cha nyuma. Alisema ameridhishwa na hali ya usalama katika ndani ya nchi hiyo na akashauri wakimbizi waanze kurejea nchini mwao ili waende kuijenga nchi yao na kushiriki kwenye masuala ya maendeleo.

Jana, Waziri Mkuu Majaliwa alitarajiwa kushiriki ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79) ambako alitarajiwa kujumuika na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa 193 na pia kutoa salamu za serikali.

Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni "Hakuna kuachwa nyuma yeyote: Kushirikiana pamoja kuendeleza amani, maendeleo endelevu na heshima ya binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo."