UDSM yaanza ujenzi wa kampasi mpya ya kilimo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:12 AM Sep 23 2024
Naibu Mratibu wa mradi huo, Dk. Liberato Haule.
Picha: Mtandao
Naibu Mratibu wa mradi huo, Dk. Liberato Haule.

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeanza ujenzi wa kampasi mpya ya kilimo mkoani Lindi.

Imeelezwa kuwa ujenzi huo utatumia miezi 18 kukamilika, ukitajwa kuleta matumaini kwa wananchi kupata fursa za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.

Ujenzi wa chuo hicho unaotekelezwa eneo la Ngongo, Kata ya Jamhuri, Manispaa ya Lindi na Kijiji cha Nandagara, wilayani Ruangwa, umefikia asilimia 20.

Naibu Mratibu wa mradi huo, Dk. Liberato Haule, akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo la Ngongo, alisema ujenzi umeanza baada ya mkandarasi kukamilisha taratibu za mkataba.

Alisema mradi huo uliopewa unaotekelezwa na mkandarasi kutoka Jamhuri ya Watu wa China, unagharimu Sh. bilioni 13, fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB).

Alisema kuwa ujenzi wa mradi huo ulianza mwezi Julai mwaka huu, ukitarajiwa kukamilika Desemba mwakani, ukihusisha vyumba sita vya madarasa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 60 kila moja.

Msimamizi wa mradi huo kutoka UDSM, Bahati Thomas, akielezea maendeleo ya ujenzi, alisema unakwenda vizuri, huku akitaja changamoto inayowakabili ni pamoja na upatikanaji saruji kutoka Kampuni ya Dangote ya Mtwara.

"Tunashukuru kazi inakwenda vizuri, changamoto yetu ni upatikanaji wa saruji kutoka Dangote kutokana na kuzidiwa na uhitaji wa wateja," alisema Thomas.

Baadhi ya vibarua wanaoshiriki katika mradi huo, wakiwamo Abdallah Juma, Alphonce Ngajira na Mwajuma Selemani, walishukuru serikali kupeleka fursa hiyo mkoani Lindi'  inawasaidia kubadilisha hali zao kiuchumi.