Madalali wa Mahakama waaswa kutekeleza vema majukumu yao kuepuka kulalamikiwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:15 PM Sep 23 2024
Msajili wa Mahakama ya Rufani George Herbert
Picha: Mpigapicha Wetu
Msajili wa Mahakama ya Rufani George Herbert

Msajili wa Mahakama ya Rufani George Herbert ametoa wito kwa madalali na wasambaza nyaraka za Mahakama kutekeleza vema majukumu yao ili kuepuka malalamiko ya wananchi ambayo yataleta athari hasi kwa Mahakama, wao binafsi, familia na taifa kwa ujumla.

Herbert ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya 13 ya watu wenye nia ya kufanya kazi ya Udalali na Usambazaji wa Nyaraka za Mahakama zaidi ya 27 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini, leo tarehe 23/09/2024 katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania), jijini Dar es Salaam.

“Endapo mtafanikiwa kuhitimu mafunzo yenu na kusajiliwa mtakuwa maafisa wa Mahakama ambao mtapewa jukumu la kutekeleza amri halali za Mahakama. Jukumu hilo msipolitekeleza vyema mtalalamikiwa kwa kutokuwatendea haki wananchi na kwa hiyo ni dhahiri kuwa Mahakama pia itakuwa imelalamikiwa,” amesema Herbert.

Vilevile Msajili huyo amewakumbusha washiriki hao kuwa kosa dogo linaloweza kujitokeza katika utendaji wao wa kazi halitakuwa madhara kwao peke yao bali litakuwa na madhara kwa familia zao, Mahakama na taifa kwa ujumla, hivyo wanapaswa kuzingatia kanuni, taratibu, miongozo na maadili ya kazi yao.

Hata hivyo, Msajili  amewaambia washiriki hao kuwa kila kazi ina malalamiko lakini malalamiko hayo yatakosa uhalali endapo tu kazi hiyo itatekelezwa kwa haki na uadilifu. 

Mafunzo hayo yameandaliwa na kuendeshwa  na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambacho kimekuwa kikendesha mafunzo haya kwa mujibu wa Kanuni ya 4 na ya 6 za Kanuni za Madalali  na Wasambaza Nyaraka za Mahakama Na.363 za mwaka 2017.

Naye mratibu wa mafunzo hayo mhadhiri kutoka IJA, Fatuma Mgomba amesema kuwa malengo ya mafunzo hayo ni kuwawezesha washiriki kupata ujuzi na maarifa ili waweze kufanya shughuli hizo kwa kuzingatia kanuni, taratibu, sheria, maadili, uweledi na ufanisi.

Mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa wiki mbili hadi Septemba 07,2024, ambapo Washiriki watafanya mitihani ya kupima umahiri wao na watakaofaulu watapatiwa vyeti vya umahiri vinavyowapa sifa ya  kufanya kazi hiyo.