Mkakati matumizi ya maji kwa kuzingatia mahitaji ya kila sekta umeleta mafanikio- Kapinga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:38 PM Sep 24 2024
Mkakati matumizi ya maji kwa kuzingatia mahitaji ya kila sekta umeleta mafanikio- Kapinga

Imeelezwa kuwa, Mkakati wa ushirikiano uliowekwa na Wizara zinazohusika na Sekta ya Maji ili kutoa elimu ya kulinda vyanzo vya maji pamoja na kushirikiana na jamii kulinda vyanzo hivyo umeonesha mafanikio.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameyasema hayo leo Septemba 24, 2024 mkoani Ruvuma wakati  Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan alipozindua mradi wa maji katika eneo la Mtyangimbole ikiwa ni muendelezo wa ziara yake mkoani humo.

 Kapinga amesema  ushirikiano wa Wizara hizo hauishii katika kutoa elimu na  kuvilinda vyanzo vya maji pekee  bali wanahakikisha maji yanatumika kwa kufuata mahitaji ya kila sekta. 

Amesisitiza kuwa kwa kutambua sekta ya maji ni mtambuka, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko aliitisha kikao cha Wizara zote zinazonufaika na Sekta ya Maji kwa nia ya kuweka mikakati ya ushirikiano katika matumizi endelevu ya maji.

1

" Mfano Wizara ya Maji, Kilimo na Nishati zinategemeana kuhakikisha huduma zetu za umeme zinaenda vizuri, huduma za kuwapatia wananchi maji  zinaenda vizuri na huduma nyinginezo kama za umwagiliaji  pia zinaenda vizuri kwa kutumia vyanzo ambavyo tunavyo.' amesema Kapinga

Amesema matunda ya matumizi bora ya maji ni pamoja na mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao sasa mashine tatu tayari zinazalisha umeme kwa kutumia  maji ambapo kabla ya kuanza kwa mradi huo  uzalishaji umeme kwa kiwango kikubwa ulitemegea chanzo cha Gesi Asilia.

Kuhusu shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo kuharibu vyanzo vya maji, Kapinga amesema Taasisi zote za Serikali zinashirikiana kuhakikisha mazingira yanatunzwa pamoja na  kutoa elimu ili kuhakikisha maji hayachepushwi pasipo utaratibu.
2