Boniface kuendelea kusota rumande hadi Septemba 26

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 10:14 AM Sep 24 2024
Boniface kuendelea kusota rumande hadi Septemba 26
Picha;Mtandao
Boniface kuendelea kusota rumande hadi Septemba 26

ALIYEKUWA Meya wa Ubungo, Boniface Jacob maarufu kwa jina la ‘Boni Yai’ ameendelea kusota rumande, baada ya kushindwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa ajili ya kusomewa uamuzi wa pingamizi la dhamana yake.

Aidha, mahabusu wote wa gerezani hawakufikishwa mahakamani jana.

Kesi hiyo ilipangwa kutolewa uamuzi jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga wa mahakama hiyo, lakini imeahirisha hadi Septemba 26.

Awali, upande wa mashtaka uliwasilisha maombi mawili mbele ya mahakama hiyo ikiwamo kupinga Jacob kupewa dhamana katika mashtaka mawili yanayomkabili likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo.

Katika maombi yao wanaiomba mahakama itoe amri kwa mujibu maombi kuruhusu kupekuliwa akaunti yake ya X na kutoa nywila (password), ili kurahisisha uchunguzi wa akaunti hiyo inayoendana na makosa yake.

Ombi la pili la upande wa mashtaka, waliiomba mahakama kutotoa dhamana kwa mshtakiwa (Jocob) kwa sababu za usalama wake akiwa uraiani.

Kosa la kwanza anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo, Septemba 12, kuwa Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kwa kupotea.

Kosa la pili, ambalo lilitokea Septemba 14, 2024, linahusiana na kuchapisha taarifa nyingine za uongo zinazosomeka 'Polisi wanatesa watu na kuua ndio kazi wanaweza. 

Hata hivyo, Boniface alikana mashtaka yote hayo na upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Nasoro Katuga uliwasilisha maombi hayo mawili ambayo yalitakiwa kutolewa uamuzi wake jana.

Septemba 19, 2024 Jacob alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya kuchapisha taarifa za uongo, jopo la mawakili wa serikali liliwasilisha hoja ya kutaka anyimwe dhamana ili kulinda usalama wake.