EWURA mwenyeji mkutano RERA

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:58 PM Sep 24 2024
Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Elimu kwa Umma na Huduma kwa Wateja katika picha ya pamoja mara baada ya kikao kinachofanyika Zanzibar.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Elimu kwa Umma na Huduma kwa Wateja katika picha ya pamoja mara baada ya kikao kinachofanyika Zanzibar.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imechaguliwa kuwa mwenyeji wa vikao vya kamati ndogo za Umoja wa Mamlaka za Udhibiti wa Sekta ya Nishati Kusini mwa Afrika (RERA) kwa mwaka huu.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na EWURA, lengo mahsusi la mikutano ya RERA ni kuwezesha taasisi wanachama kubadilishana uzoefu wa udhibiti na utendaji wa sekta ya nishati katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC).

Imesema mamlaka za udhibiti kutoka Angola, Botswana, Afrika Kusini, Namibia, Lesotho, Eswatini, Zambia, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na Tanzania zimeshiriki vikao hivyo ambavyo vimeanza rasmi Septemba 23 visiwani Zanzibara hadi 27, mwaka huu.

“Kwa upande wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imeshiriki kama mtazamaji kwa kuwa bado haijawa mwanachama rasmi wa umoja huo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Pia imeeleza kuwa vikao hivyo vilivyoanza rasmi vinavoendelea visiwani Zanzibar, vinaangazia masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuboresha shughuli za udhibiti wa nishati katika maeneo ya fedha, rasilimali watu, huduma kwa wateja, habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, bei, tozo na viwango vya huduma kwenye sekta za umeme, mafuta na gesi asilia.

Aidha, imeeleza kuwa mikutano ya RERA inafanyika kwa awamu mbili, na kwamba ya kwanza ni ngazi ya watendaji, ambao wanaketi katika vikao vya kamati ndogo sita, kati ya muda uliotajwa, na ngazi ya wakuu wa taasisi wanachama wa RERA, ambao vikao vyao vitafanyika kuanzia Oktoba nane hadi 11, mwaka huu.