Rais Samia azindua maghala 28 ya kuhifadhi chakula Vijijini

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 05:51 PM Sep 24 2024
Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi maghala ya kuhifadhi nafaka mkoani Ruvuma, kushoto ni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Picha:Mpigapicha Wetu
Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi maghala ya kuhifadhi nafaka mkoani Ruvuma, kushoto ni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

RAIS Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa maghala 28 ya kuhifadhi nafaka katika eneo la ghala la Luhimba, mkoani Ruvuma.

Rais Samia ameweka jiwe hilo la msingi akiwa kwenye mwendelezo wa ziara yake mkoani humo.

Akizungumza mbele ya Rais Samia, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema wanaamini kwamba maghala hayo yatakuwa  mkombozi kwa wakulima. 

“Maghala haya 28 ni sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa maelekezo yako Rais ya kujenga maghala 70 vijijini ambayo yana uwezo wa kuhifadhi tani 1000 kila moja, na kwa ujumla ni ya tani 28000 kwa maghala yote 28,” amesema Bashe.

Bashe alisema  kazi hiyo ni utekelezaji wa mikakati ya wizara yake ya kujenga maghala vijijini.

 Amesema kuwa maghala hayo yamejengwa katika halmashauri nne za Wilaya za Songea Manispaa (ghala 1), Songea DC (maghala 11), Madaba (maghala 9) na Namtumbo (maghala 7). 

“Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) tayari imeanza kutumia maghala matano kuhudumia wakulima, kati ya maghala 28 ambapo kutakuwa na maghala mengine matano yanayotarajiwa kukamilika wiki chache zijazo,” amesema Bashe. 

Bashe alisema gharama za ujenzi wa maghala 28 ni Sh. bilioni 14.7 ambayo ni gharama ya Sh. milioni 527 kwa kila ghala. 

Kadhalika, alimwelezea Rais Dk. Samia kuwa NFRA nayo inatarajia kujenga maghala makubwa ya kısasa yenye uwezo wa kuchukua tani 5000 kila ghala. 


Alisema maghala hayo yatajengwa kwenye miji ya mikoa mitano ya uzalishaji wa mazao ya Katavi, Rukwa, Ruvuma, Songwe na Tabora.