Maliasili, Mambo ya Ndani zatakiwa kushirikiana kukuza utalii

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:13 PM Jan 14 2025
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana.
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana.

Wizara ya Maliasili na Utalii imetakiwa kushirikiana kwa ukaribu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kukuza soko la utalii nchini na kurahisisha utoaji wa huduma ya viza kwa watalii.

Hayo yamesemwa leo Januari 14,2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava katika kikao kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.

“Wizara ya Mambo ya Ndani, Uhamiaji na Wizara ya Maliasili na Utalii mshirikiane kuikuza Sekta ya Utalii, tunahitaji mfanye zaidi kuisaidia sekta hii na kama kuna changamoto mkazitatue”  Mnzava amesisitiza.

Mnzava amezitaka Wizara hizo kuoanisha mifumo ya malipo kwa watalii na kuweka mikakati madhubuti ya kutambua masoko muhimu ya watalii na kuwavuta waje nchini sambamba na kurahisisha michakato ya kupata viza kwa  watalii hao.


Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana ameiahidi  kamati hiyo kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii itahakikisha inafanya kazi kwa ukaribu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha soko la utalii linakua ili kuunga mkono juhudi za Rais  Dk. Samia Suluhu Hassan za kukuza Sekta ya Utalii nchini.

“Tutahakikisha tunatambua masoko muhimu ya utalii na kuweka mikakati madhubuti ya kuvutia watalii kwa kushirikiana ”Chana amesema.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Viongozi na Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake pamoja na Viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ndani ya Nchi na Uhamiaji.