WALIMU wamekumbushwa kuweka mazingira ambayo yanampa fursa mtoto wa kike kujifunza uongozi kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha katika shughuli za shule, taasisi za umma na binafsi.
Imeelezwa kuwa hatua hiyo itawasaidia kupata uzoefu wangali wadogo lakini pia kujiamini na kufanya jambo kwa ufanisi.
Hayo yamesemwa leo na msimamizi wa klabu za kupinga ukatili shuleni, Halima Masoud kutoka Kituo cha Taarifa na Maarifa Majohe jijini Dar es Salaam, ambacho kipo chini ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Msimamizi huyo alikuwa akizungumza na wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Mji Mpya iliyopo Kata Majohe, katika kilele cha Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani.
"Tunapaswa kumfundisha mtoto wa kike kujitambua, kujisimamia na kuwa na ujasiri wa kuongoza, kwani uongozi unahitani kujiamini. Jukumu letu ni kuhakikisha mtoto wa kike anapata mazingira yanayosaidia kukuza aifa hizo " amesema Halima.
Mwalimu Mary Kwinga ambaye anasimama klabu ya jinsia shuleni hapo, amesema kwa kushirikiana na Kituo cha Taarifa na Maarifa Majohe, wamesaidia wanafunzi kujitambua kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
Amesema awali kulikuwa na matukio mengi ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi, uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watu wa mitaani lakini sasa umepungua.
"Tumewafundisha watoto jinsi ya kutoa taarifa za matukio hayo Kwa kushirikiana na Kituo cha Taarifa na Maarifa Majohe, sasa kukiwa na viashiria ya vitendo, wanatoa taarifa kwetu " amesema Mary.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Abubakar Shauri amesema shule hiyo haina uzio, na kwamba inakuwa rahisi hata kwa vijana wa kihuni kupita katika mazingira ya shule.
"Lakini kwa kuwa tayari wanafunzi wana elimu ya jinsi ya kutoa wahuni, imekuwa ni rahisi kuwadhibiti, lakini pamoja na hayo, shule kuwa na uzio ni jambo muhimu " amesema Shauri.
Amesema shule hiyo yenye wanafunzi 3131 ikiwa na uzio itakuwa ni rahisi pia kudhibiti utoro.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED