DC Sima awahimiza wazazi kuwapeleka watoto shuleni

By Restuta Damian , Nipashe
Published at 07:27 PM Jan 13 2025
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Erasto Sima.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Erasto Sima.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Erasto Sima, amewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao wanaostahili kuanza elimu ya shule ya awali, darasa la kwanza, na kidato cha kwanza katika shule walizochaguliwa ili kuongeza idadi ya wanafunzi shuleni.

Akizungumza na vyombo vya habari leo, wakati wa ufunguzi wa mhula wa masomo kwa mwaka 2025, Sima alisema wilaya ya Bukoba ina halmashauri mbili na kata 43, ikiwa ni Manispaa ya Bukoba (kata 14) na Bukoba vijijini (kata 29).

Alieleza kuwa, mwaka 2024, wanafunzi 9,231 wa darasa la saba walifanya mtihani wilayani Bukoba, ambapo wavulana walikuwa 4,483 na wasichana 4,749. Kwa mwaka huu, ufaulu umefikia wanafunzi 6,339, ikiwa ni wavulana 3,050 na wasichana 3,348.

Aidha, alisema baadhi ya wazazi walishaanza maandalizi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa watoto wao katika shule za Serikali na binafsi. Hadi Januari 10, 2025, wazazi walikuwa wametwaa fomu 4,780 kwa shule mbalimbali wilayani Bukoba.

Kuhusu watoto wanaojiunga na darasa la awali na darasa la kwanza, alisema zaidi ya asilimia 70 ya watoto wameandikishwa, ambapo watoto 6,543 kati ya 8,959 wamejiandikisha, na darasa la kwanza lina wanafunzi 6,188 kati ya 8,947.