CCM wakutana kujadili tuhuma za Waitara

By Ambrose Wantaigwa , Nipashe
Published at 08:55 AM Feb 19 2025
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.
Picha: Mtandao
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kimeketi kikao maalumu kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ikiwamo tuhuma zilizotolewa na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.

Wiki iliyopita Waitara akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa bunge mkoani Dodoma alidai kuwa kuna wanachama wanaomuunga mkono wanatishiwa maisha na wengine wamepotea.

Pia, alidai kuna viongozi kadhaa wa matawi na kata jimboni humo walitekwa na kutishiwa maisha kutokana na kumuunga mkono.

Katika mahojiano hayo mbunge huyo aliwataja kwa majina waathirika wa vitisho hivyo, huku akiomba chama hicho kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua wahusika wa vitisho hivyo.

Akithibitisha kufanyika kwa kikao hicho juzi alipozungumza na Nipashe kwa njia ya simu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi alisema kikao hicho kimefanyika mjini Tarime ingawa hakuweka wazi ajenda nyingine zilizojadiliwa katika kikao hicho. 

"Ndio tumesikia tuhuma hizo kama watu wengine kwenye mitandao ya kijamii, tumekutana Jumapili Tarime kujadili suala hilo kupitia vikao halali kama ulivyo utamaduni wa chama chetu, tutatoa taarifa baadaye kwa vyombo vya habari," alisema Chandi.

Mbio za kuwania jimbo hilo zimeshika kasi kuelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu ambapo mbunge huyo ameshatangaza nia ya kutetea kiti hicho mara ya pili baada ya kumshinda Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche katika uchaguzi wa 2020.

Hadi sasa Heche naye ametangaza nia ya kuwania kuteuliwa na chama chake kugombea kiti hicho, huku makada mbalimbali wa CCM wakipewa nafasi ikiwa ni pamoja Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi na aliyewahi kuwa Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine.