Bashungwa ataka ujenzi barabara ya Nyamwage-Utete ukamilike kwa wakati

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 09:13 PM Oct 24 2024
WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa.
Picha:Mpigapicha Wetu
WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa.

WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa amemuagiza mkandarasi wa Kampuni ya China Railways seventh Group Limited (CRSG ) kuhakikisha anajenga barabara ya Nyamwage -Utete yenye urefu wa Km 33.7 kulingana na mkataba aliousaini.

Bashungwa amesema kutokana na umuhimu wa barabara hiyo mkandarasi anatakiwa kutokuwa sababu ya kuchelewesha ujenzi  wake pamoja na kuzingatia jitihada za Serikali kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo 

Amesema mkandarasi huyo anatakiwa kuwa na vifaa vyote vinavyotakiwa kuwepo eneo la mradi kwa asilimia 100 kulingana na mkataba aliousaini na kuhakikisha kasi ya ujenzi inaongezeka kwa kuzingatia umuhimu wa barabara..

"Meneja wa TANROADS hakikisha huyu mkandarasi ana vifaa vyote vinavyotakiwa akiwa eneo la mradi hatutaki kujua yeye anaishi wapi tunataka vifaa vyote vilivyopo kwenye mkataba vinaonekana eneo la ujenzi na wataalamu wa kutusha hii barabara ni muhimu sana na inatakiwa kukamilika kwa wakati uliopangwa," amesema

Vile vile Waziri huyo amesema Serikali Ina Mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Nyamwage Utete hadi Chalinze ambayo itawarahisishia safari wakazi wa mikoa ya kusini ambao hawana ulazima wa kupitia Mkoa wa Dar es Salam.

Awali Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage amesema utekelezaji wa mradi huo ambao mkataba wake ulisainiwa 2022 hadi sasa umefikia asilimia saba.

1

Mhandisi Mwambage amesema wanaendelea kumsimamia kwa karibu mkandarasi huyo ambaye hivi karibuni ameonyesha kusuasua kwenye ujenzi wa barabara hiyo ambayo inategemewa na wananchi walio wengi kufungua uchumi wao pindi wanaposafirisha bidhaa wanazozalisha.

Barabara ya Nyamwage - Utete ambayo inafika yalipo makao makuu ya Wilaya ya Rufiji tangu Uhuru wananchi wake wamekuwa wakiwasilisha ombi lao la ujenzi wa kiwango cha lami ambao kwasasa ndio utekelezaji wake umeanza na unaokwenda kurahisisha usafiri.

Akiwa Rufiji Bashungwa pia ametenbelea na kukagua ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Utete ambayo ilijengwa miaka zaidi ya 50 iliyopita, na pia akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Rufiji baada ya kuweka jiwe la Msingi huku akiwasisitiza kusoma kwa bidii baada ya kuboreshewa miundombinu.
2

Katika ziara yake Wilaya ya Kibiti ameweka jiwe la Msingi katika shule ya Sekondari Wananchi, Sekondari ya Dt Samia Lumyozi ambazo zimejengwa kuwapunguzia adha wanafunzi kutembea umbali mrefu na kuzungumza na wananchi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibiti Juma Ndaruke ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuidhinisha fedha za miradi ya maendeleo ambayo inatatua kero za wananchi.