TCRA kumaliza laini ‘tuma kwa namba hii’

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 11:11 AM Oct 24 2024
Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA, Mhandisi Felician Mwesigwa
Picha:Mtandao
Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA, Mhandisi Felician Mwesigwa

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema inaendelea kushughulikia laini za simu zinazotumika kufanya utapeli wa mtandao ili kuzimaliza kabisa.

Katika kufanya hivyo, TCRA imesisitiza kuwa kila ujumbe mfupi wa maneno ‘sms’ utakaotumwa utarekodiwa.

Akitoa wasilisho la Ripoti ya Tathmini ya Mawasiliano Tanzania inayoanzia Juni hadi Septemba, mwaka huu, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA, Mhandisi Felician Mwesigwa, huku akiwanyoshea kidole mawakala wasio waaminifu wanaosajili laini kwa njia ambazo ni kinyume na utaratibu.

Ripoti hiyo ilionesha kuwa mikoa ya Rukwa na Morogoro imeongoza kwa kuwa na majaribio ya ulaghai wa kimtandao huku ikibainisha kuwa katika maeneo mengine matukio hayo yamepungua kwa asilimia 28, ikilinganishwa na yaliyoripotiwa katika ripoti ya Juni, mwaka huu.

“Mikoa hiyo imeongoza mwaka mzima. Kuna mtu anaamua kusajili laini ya simu ili akafanye kile anachoona ni fursa kwake. Mtu anajua kabisa kwamba nikifanya kosa kuna sheria zake lakini bado anafanya, hivyo kazi yetu sisi ni kuhakikisha upatikanaji wa laini hizo usiwe rahisi.

“Watoa huduma wengi wametumia teknolojia za kubaini hizo ‘sms’ na kuzifungia laini husika pia kuwaangaliwa wale ambao wamesajili laini hizo zilizotumika kwenye kufanya matukio ya kitapeli. Hiyo inakwenda sambamba na hatua mbalimbali za udhibiti,” alisema Mwesigwa.

Ripoti hiyo ambayo hutolewa na TCRA kila baada ya miezi mitatu, ilionesha kwamba mikoa hiyo imeongoza kwa kuwa na theluthi moja ya majaribio ya ulaghai kupitia simu za mkononi kwa kutumwa ujumbe mfupi wa maneno mfano ‘hiyo fedha nitumie kwa namba hii 0713 46... jina litatoka ...).

Njia nyingine ya utapeli inayotumika katika maeneo hayo, ilielezwa kuwa ni tapeli kumpigia simu ya moja kwa moja mtu mwingine na kujitambulisha kuwa ni mtoa huduma wa mtandao fulani na kumpa maelekezo ambayo endapo mhusika atayafuata yatasababisha kutapeliwa.

Kutokana na hali hiyo mitandao mbalimbali ya laini za simu imekuwa ikitoa elimu na msisitizo kwa wateja kwamba watawasiliana nao kwa namba 100 pekee, hivyo wajiepushe na kufuata maelekezo yoyote watakayopatiwa na mtu aliyewapigia kwa namba binafsi.

“Kila mwaka kwenye ripoti zetu, mikoa ya Rukwa na Morogoro imekuwa na matukio mengi ya ulaghai. Wilaya zilizoongoza kwa Rukwa na matukio yake kwenye mabano ni Simbawanga (5,198), Nkasi (250) na Kalambo (122) huku Morogoro zikiwa ni Ifakara (3,922), Kilombero (1,306), Morogoro (127), Kilosa (89), Ulanga (21), Mvomero (10), Malinyi (manane) na Gairo (matatu).

Mhandisi Mwesigwa pia alitaja mikoa iliyofuatia kwa matukio ya majaribio ya utapeli baada ya Rukwa na Morogoro kuwa ni Mbeya (1,112), Dar es Salaam (959) na Arusha (351) ambayo yalifanyika kwa wastani wa asilimia moja hadi 10.

Kuhusu sababu za mikoa hiyo kuongoza, alisema chanzo chake kilitokana na wahusika kutekeleza wakiwa katika maeneo hayo.