Bashungwa aiagiza TANROADS kutafuta fedha kukamilisha ujenzi wa barabara Mkuranga

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 07:16 AM Oct 24 2024
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa
Picha: Julieth Mkireri
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amemuagiza Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara TANROADS, Doroth Mtenga kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha Kilometa 1 ya barabara inayoelekea Bandari ya Kisiju Mkuranga ambayo imesimama kwa zaidi ya miezi tisa.

3Waziri Bashungwa ametoa maagizo hayo alipofanya ziara katika Wilaya ya Mkuranga kukagua miradi ya maendeleo ambapo alisema barabara za Mkuranga ni za  Wilaya za Viwanda hivyo Wizara inawajibika kuziweka kwenye barabara za kimkakati kurahisisha usafirishaji.


Bashungwa alisema Kaimu Mtendaji Mkuu huyo atatakiwa kuhakikisha fedha kwa ajili ya Kilometa zilizobaki kufikia saba zinapatikana na kukamilisha ujenzi ili baadae wizara ifanye mipango kwa ajili ya kumaliza Km 38 zilizobaki kujengwa kwa kiwango cha lami kati ya 45 zilizopo.


Awali Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage akiwasilisha taarifa ya barabara hiyo alisema barabara ya Mkuranga Kisiju yenye urefu wa km 45. kwasasa ni Km sita pekee  zimejengwa kwa kiwango cha lami na km moja inasubiri fedha kukamilisha km saba.

1

Kwa mujibu wa Meneja huyo endapo barabara hiyo yote itajengwa kwa kiwango cha lami itarahisisha usafiri kuelekea bandari ya Kisiju  na pia itafungua shughuli za kiuchumi.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Hadija Nasri aliomba Serikali kutenga fedha kwa ajili ya barabara hiyo ya kimkakati  inayoelekea kwenye kongano ya viwanda lilipotengwa eneo la uwekezaji.