Mwambusi atua Coastal Union

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:38 AM Oct 24 2024
   Mwambusi atua Coastal Union
Picha:Mtandao
Mwambusi atua Coastal Union

KOCHA wa zamani wa Mbeya City, Ihefu na Yanga, Juma Mwambusi, ameanza kazi rasmi ya kuifundisha Coastal Union, klabu hiyo imethibitisha.

Mwambusi aliyehudumu kama Kocha Msaidizi wa Yanga chini ya Mholanzi, Hans van Pluijm, amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu hiyo yenye maskani yake jijini Tanga.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa habari wa Coastal Union, Abass El Sabri, alisema uongozi una matumaini na kocha huyo kutokana na uzoefu wake katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Ni kweli tumemalizana na Kocha Mwambusi, ameanza kazi ya kukinoa kikosi chetu, tunaamini kwa uwezo wake na uzoefu wa Ligi Kuu, timu yetu ipo kwenye mikono salama na tunaweza kufanya vizuri," alisema Sabri.

Mwambusi amejiunga na Coastal Union akichukua mikoba iliyoachwa na David Ouma, ambaye alitimuliwa tangu Agosti mwaka huu kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Kocha huyo anaanza kibarua huku Coastal Union yenye pointi nane ikiwa kwenye nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo vinara ni Singida Black Stars wenye pointi 19.