Waliyoiba fedha za kanisa wasota rumande, upelelezi bado

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 12:56 PM Oct 24 2024
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Picha: Mtandao
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

UPELELEZI wa kesi ya wizi wa fedha za Kanisa la Sabato Tanzania (SDA) wa Sh. milioni 717.1 inayomkabili Ofisa TEHAMA wa Kanisa hilo, Wilson Mapande na wenzake wawili haujakamilika.

Aidha, mshtakiwa Mapande na Winnie Owino (33), wanatuhumiwa kati ya Mei, 2021 na Januari, 2023 walitumia fedha  hizo kununua magari mawili  aina ya Toyota Harrier, Toyota Crown na pia walinunua nyumba katika eneo  ambalo halijapimwa  Mtaa wa Mtambani, Mapinga  Bagamoyo.

Taarifa hiyo ya upelelezi imetolewa na Wakili wa Serikali, Asiath Mzamiru mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Maximilian Malewo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Mzamiru amedai kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa, ambapo upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika,  hivyo aliomba tarehe nyingine ya kutajwa ili kuangalia hatua ya upelelezi ilipofikia.

Baada ya kudai hayo, Hakimu Malewo, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 6,  mwaka huu kwa kutajwa, washtakiwa wamerudishwa rumande kwa sababu shtaka la utakatishaji fedha kisheria halina dhamana.

Mbali na Mapande, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa Kanisa hilo, Owinona mfanyabiashara Nicolaus Owino(29) ambao walipanda kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Maximilian Malewo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka manane, kuongoza genge la uhalifu, wizi na mashtaka yote yaliyobaki ni utakatishaji fedha. 

Inadaiwa kuwa katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanatuhumiwa kati ya Mei, 2021 na Januari, 2023, jijini Dar es Salaam waliongoza genge la uhalifu kisha kujipatia Sh. Milioni 717, 126,245, kutoka akaunti ya  benki ya CRDB,  mali ya kanisa hilo.

Katika shtaka la pili Mshtakiwa Mapande  anadaiwa kati ya Mei, 2021 na Januari, 2023, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa mtumishi wa Kanisa hilo aliiba Sh.  milioni 717.1, mali ya Kanisa.

Inadaiwa kuwa katika shtaka la tatu la utakatishaji fedha, inadaiwa kati ya Mei, 2021 na Januari, 2023 Mapande alifungua akaunti benki ya CRDB lenye jina lake kisha akaingiza sh. milioni 396, 629,029.

Shtaka  la nne linawakabili  Mapande na Winnie, inadaiwa  katika kipindi hicho walifungua akaunti benki ya CRDB, yenye jina la Winnie, kisha wakaingiza sh. milioni 208,468, 091.

Pia, katika shtaka la tano, linamkabili Mapande na Owino, inadaiwa washtakiwa hao walifungua akaunti benki hiyo na kuingiza Sh. 112, 029,123, lenye jina la Owino.