‘TACAIDS iongeze kasi huduma VVU/UKIMWI jamii za wavuvi’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:59 AM Oct 24 2024
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dk. Christina Mzava.
Picha:Mtandao
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dk. Christina Mzava.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeagiza Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kuongeza kasi ya utoaji elimu ya kujikinga na Virusi vya UKIMWI (VVU), huduma za kinga, matibabu na matunzo miongoni mwa wavuvi katika maziwa na bahari.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dk. Christina Mzava pamoja na kamati yake walisema juzi jijini hapa kuwa elimu ya kujikinga na VVU miongoni mwa jamii ya wavuvi ipo chini, hali kadhalika upatikanaji huduma za VVU na UKIMWI si wa kuridhisha.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, wakijadili baada ya taarifa ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega kuwasilishwa kwa kamati hiyo kuhusu hatua za ujumuishaji afua za VVU na UKIMWI kwenye sekta ya uvuvi, walisema elimu ya kujikinga na VVU, pamoja na huduma za kinga, matibabu na matunzo miongoni mwa wavuvi bado zinahitaji kuongeza kasi kwa kuwa hali ya maambukizi kwa wavuvi bado ipo juu.

Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Christina Mzava, alisema TACAIDS ina kazi kubwa ya kufanya katika sehemu za mialo ili kuokoa jamii za wavuvi kutokana na kuwa na ushamiri wa juu wa VVU kwa asilimia saba ambayo ni zaidi ya kiwango cha kitaifa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Samweli Mwashamba, akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa niaba ya Waziri Ulega, alisema wizara na taasisi zake 10 inaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji afua za VVU, UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukizwa (MSY) mahala pa kazi kwa mujibu wa Waraka Na 2 wa Utumishi wa Umma wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na MSY Mahala pa Kazi katika Utumishi wa Umma wa Mwaka 2014.

Alitaja maeneo yanayotekelezwa na wizara hiyo kuwa ni pamoja na kujumuisha masuala ya uvuvi na UKIMWI katika Sera ya UVUVI ya Mwaka 2015, kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji masuala ya kudhibiti VVU na UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza, kutoa elimu lishe na upimaji wa hiari kwa watumishi pamoja na kaanzisha vituo vya upimaji na ushauri nasaha kwa wavuvi.

Pia aligusia kuunda Kamati ya VVU na UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza pamoja na kuwa na mratibu wa UKIMWI, usambazaji makasha ya kuhifadhi kondomu na kondomu katika maeneo ya kazi ya wizara.

Alitaja sababu zinazochangia jamii za wavuvi kuwa na maambukizi ya VVU ni pamoja na matumizi hafifu na yasiyo sahihi ya kondomu na imani mbovu za kutoamini kondomu kwamba zinaweza kutumika na kuleta furaha ya tendo. 

Pia kuna uelewa mdogo juu ya elimu ya VVU na UKIMWI katika kambi za wavuvi ambao hupelekea kufanyika ngono zisizo salama pamoja na kutokuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kuwa na ufahamu wa afya zao pamoja na upatikanaji hafifu wa huduma za VVU na UKIMWI katika maeneo ya mialo hasa visiwani.

Alisema kuwa wanafanya pia sensa za wavuvi ili kuweka mkakati wa namna ya kutoa huduma za upimaji na ushauri nasaha, huduma za VVU na UKIMWI zinazotolewa asilimia 51 katika mialo 1,307.

Samweli Mwashamba alifafanua kuwa jumla ya kondomu 334,872 na makasha 30 ya kuhifadhi kondomu yamesambazwa kwenye wizara na taasisi zake katika kipindi cha mwaka 2023/24. Lishe na nauli kwa watumishi wa wizara na taasisi ambao waliojiweka wazi kuwa wanaishi na VVU katika kipindi cha mwaka 2023/24.

Watumishi 387 walipatiwa elimu ya juu ya VVU na UKIMWI na ushauri nasaha pamoja na kufanyiwa vipimo.