Ester Thomas: Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Watiania msikubali kutishwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:30 PM Oct 24 2024
Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Bara, Ester Thomas.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Bara, Ester Thomas.

Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Bara, Ester Thomas amesema ACT Wazalendo imejipanga vyema kuhakikisha wanachama wake waliotia nia kugombea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wanapata msaada wa kisheria katika kipindi cha uhitaji.

Alisema maneno hayo jana Oktoba 23 Jijini Mwanza wakati akizungumza na watia nia wa mitaa ya majimbo ya  Nyamagana na Ilemela.

"Madhali umetia nia kugombea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Naomba simama imara, usitetereke, usiwe na hofu na wala usikubali kutishwa. Chama kiko pamoja na wewe. Pia tuna Wanasheria; ambao wako tayari kukusaidia wakati wowote." alisema Ester 

Aidha Ester aliwakumbusha watia nia hao dhima na wajibu wa Mwenyekiti wa Mtaa kwenye maendeleo ya mtaa. Amesema kwenye mitaa na vijiji ndiko wanakoishi wananchi na huko ndiko inapopita na kufanyika miradi ya maendeleo.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji utafanyika Novemba 27, 2024 na ACT Wazalendo ni miongoni mwa vyama vinavyokwenda kushiriki uchaguzi huo.