Che Malone, Bacca vitani Ligi Kuu Bara 2024/2025

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:35 AM Oct 24 2024
   Che Malone, Bacca vitani  Ligi Kuu Bara 2024/2025
Picha:Mtandao
Che Malone, Bacca vitani Ligi Kuu Bara 2024/2025

MBALI na timu kupigania ubingwa, kusaka kiatu cha dhahabu, kutoa pasi za mwisho, 'asisti' na hata 'clean sheets' kwa makipa, kumezuka vita nyingine ya mabeki wa kati wa Simba na Yanga, Che Malone Fondoh na Ibrahim Hamad 'Bacca', kushindana kufunga mabao katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, inayoendelea.

Bao la dakika ya nne alilofunga kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya juzi limemfanya beki wa Simba, raia wa Cameroon, Che Malone, kumfikia Bacca ambaye amefunga mabao mawili mpaka sasa kwenye ligi hiyo.

Che Malone alitumia makosa ya kipa, Mussa Mbisa wa Prisons kushindwa kuukamata mpira vizuri, ukamponyoka na kuelekea langoni, licha ya juhudi zake za kuurukia na kutaka kuudaka kushindikana, lakini mguu wa kushoto wa Che Malone ulifanikiwa kuukwamisha wavuni.

Lilikuwa ni bao pekee katika mchezo huo likiipa Simba pointi tatu muhimu za ugenini dhidi ya Prisons, ambayo msimu uliopita iliondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wekundi wa Msimbazi.

"Lengo lilikuwa kushinda mchezo, kazi yangu ni kulinda, lakini kuna wakati naenda kusaidia washambuliaji, siwezi kusema kama nafanya hivi peke yangu, soka ni kundi, ni mchezo wa watu wengi, hivyo na mimi nawapongeza wachezaji wenzangu kwa kuipambania timu.

Nimefunga, nimezuia, tumepata ushindi, nimekuwa mchezaji bora, siku zote timu kubwa haiwezi kupoteza mechi au pointi mara kwa mara, tulipoteza mchezo uliopita, lakini leo (juzi), tumesawazisha makosa," alisema beki huyo wakati akikabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa mechi hiyo.

Bao lake la kwanza alilifunga Agosti 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, alipopachika kwa kichwa dakika ya 13, akiiongoza Simba kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United.

Bacca, ambaye na yeye ana mabao mawili, alifunga Septemba 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Yanga ikiifunga Prisons bao 1-0, kabla ya Oktoba 3 kupachika goli lingine kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam dhidi ya Pamba, timu yake ikiondoka na ushindi wa mabao 4-0.

"Mwaka huu naingia rasmi katika kinyang'anyiro cha kusaka kiatu cha dhahabu, mastraika wote hata wa Yanga wajiandae," alisema Bacca.