Fadlu: Kipa Prisons amepunguza mabao

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:30 AM Oct 24 2024
KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davis.
Picha:Mtandao
KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davis.

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davis, amemtaja kipa wa Prisons, Mussa Mbisa, ndiye aliyewanyima ushindi mnono katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya juzi.

Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 katika mechi hiyo, shukrani beki wa kati, Che Malone Fondoh, ambaye alimalizia mpira uliotemwa na Mbisa.

Hata hivyo, Mbisa ndiye aliyekuwa shujaa wa mchezo huo kwa kuokoa mashambulizi mbalimbali yaliyomlenga na kuifanya Simba kupata ushindi mwembamba katika mchezo huo.

Uimara wa kipa huyo uliokoa Simba kufunga mabao mengine mawili ya wazi katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi, Amina Kyando, kutoka mkoani Morogoro.

"Kilikuwa kiwango kizuri mno kwa kipa wao, alikuwa shujaa kwa sababu aliokoa hatari nyingi ambazo zingekuwa mabao, licha ya kufanya makosa na kupatikana bao, lakini huyo ndiye aliyesababisha wasipigwe nyingi," alisema Fadlu.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini alilalamika Uwanja wa Sokoine haukuwa katika ubora unaotakiwa hivyo kuwafanya wachezaji wake washindwe kuanzisha zaidi mashambulizi kutoka nyuma kwa kuhofia kuupoteza kutokana na changamoto hiyo.

"Tumecheza mechi kwenye kiwanja ambacho hakikuwa vizuri, ilibidi kukimbizana na kusaka mpira inayodunda, Mohamed Hussein 'Tshabalala' na Kibu Denis wamekuwa wachovu kwa sababu wametoka kwenye kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), hawajapumzika na wamecheza kiasi cha michezo sita kwa muda mfupi tu," Fadlu alisema.

Aliongeza amefurahi kupata ushindi huo pamoja uliotokana na wachezaji wake kupambana.

"Ninachofurahi tumepata ushindi kwenye mchezo mgumu, tumecheza vizuri, tumetengeneza nafasi nyingi, nadhani hiki kilikuwa ndiyo muhimu zaidi," alisema kocha huyo.

Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema haukuwa mchezo rahisi kwa sababu Prisons walikuwa bora katika kuzuia mashambulizi yao.

"Ili uifunge Prisons ni lazima wafanye makosa ndiyo uyatumie, jana (juzi), tulinufaika na makosa yao, tunasema haikuwa rahisi kushinda kulingana na ufinyu wa ratiba na wingi wa mechi mfululizo, pamoja na aina ya mpinzani tuliyecheza naye," alisema Ahmed.

Naye Kocha Mkuu wa Prisons, Mbwana Makata, alisema kama si kosa alilofanya Mbisa, basi matokeo yangekuwa tofauti.

"Udhaifu wa golikipa kudaka mpira ndiyo uliotugharimu, ila uimara katika ulinzi ulikuwa mzuri, Simba walishindwa kupata mianya, tukawa tunawanyima muda wa kuandaa mashambulizi, wakabadilika wakaanza kucheza mipira mirefu.

Nasema leo (juzi), timu iliimarika zaidi na kama isingekuwa makosa ya kipa, nadhani hadithi ingekuwa nyingine," alisema kocha huyo.

Simba sasa imefikisha pointi 16, ikishinda michezo mitano, sare moja na kupoteza mmoja, huku Prisons ikiwa katika nafasi ya 12 ikisalia na pointi saba kibindoni baada ya kushuka dimbani mara nane.