Gamondi atambia ubora kikosi chake

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:25 AM Oct 24 2024
news
Picha: Mtandao
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Clatous Chama (kushoto), akiwania mpira dhidi ya winga wa JKT Tanzania, Shiza Kichuya, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam juzi usiku. Yanga ilishinda mabao 2-0.

BAADA ya timu yake kuendelea kupata ushindi mfululizo katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema ubora wa wachezaji walioko katika kikosi chake ndio unaamua mechi.

Ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam juzi uliifanya Yanga kutimiza michezo 22 bila kufungwa, katika mashindano yote waliyocheza. 

Matokeo hayo yaliwafanya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kufikisha pointi 18 baada ya kucheza michezi sita na kupanda hadi nafasi ya pili huku vinara wakiwa ni Singida Black Stars yenye pointi 19, lakini wamecheza mchezo mmoja zaidi.

Simba yenye pointi 16 na imeshuka dimbani katika michezo saba iko kwenye nafasi ya tatu ikifuatiwa na Fountain Gate yenye pointi kama hizo, lakini imecheza mechi nane.

Akizungumza na gazeti hili jana, Gamondi, alisema timu yake imecheza mechi mbili ngumu mfululizo dhidi ya Simba na JKT Tanzania, lakini matokeo mazuri waliyapata yanatokana na ubora pamoja na viwango 'vikubwa' vya wachezaji wake.

Gamondi alisema anafurahishwa na viwango vinavyoonyeshwa na wachezaji wake katika kila mechi wanayoshuka uwanjani.

"Tumecheza mechi mbili ngumu, tulianza dhidi ya Simba na siku chache baadaye tunakutana na JKT ambayo ni timu ngumu, nashukuru wachezaji wamepambana na tumefanikiwa kupata ushindi," alisema Gamondi.

Kocha huyo alisema katika mchezo huo wa juzi walifanikiwa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza na kupelekea kupata mabao hayo mawili.

"Kipindi cha pili wapinzani wetu licha ya kuwa pungufu, walirudi uwanjani na nguvu kubwa, walicheza vizuri na kujaribu kutengeneza nafasi, lakini kama nilivyosema ubora wa wachezaji wangu umeamua mechi," alitamba Gamondi.

Kocha huyo raia wa Argentina alisema kwa sasa wanaelekeza nguvu yao katika mechi inayofuata ambapo watawafuata wenyeji Coastal Union kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

"Mechi hii imemalizika, sasa akili na mipango yetu tunaangalia mchezo unaofuata, hakuna mechi rahisi kwa sababu kila timu inahitaji kupata pointi, tutaendelea kupambana kila idara ili kutimiza malengo yetu," Gamondi aliongeza.

Naye Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, alisema timu yake ilipoteza utulivu na hali hiyo iliwapa nafasi wapinzani wao kupata mabao yaliyowapa ushindi.

Ally alisema pia kadi nyekundu iliyotolewa na kipa wake chaguo la kwanza, Denis Richard, kuliwafanya wabadilishe mpango wa mechi hiyo ambao waliingia nao.

Hata hivyo anasema anasikitika kuona wachezaji wake wamepoteza nafasi mbili za wazi za kufunga mabao ambazo walitengeneza katika mchezo huo.

Coastal Union ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo wamehamia Arusha kwa sababu uwanja wao wa asili wa CCM Mkwakwani ulioko jijini Tanga unafanyiwa ukarabati.

Mechi nyingine za Ligi Kuu Tanzania Bara zinatarajia kuchezwa kesho kwa Singida Black Stars kuwakaribisha Fountain Gate wakati Namungo itawafuata Simba na Azam FC itawaalika KenGold kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.