SADC kuuweka ‘kitimoto’ mzozo wa DRC leo, Rais Samia atia timu Harare

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:54 PM Jan 31 2025
SADC.
Photo: Mtandao
SADC.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) leo, Januari 31, 2024, inakutana mjini Harare, Zimbabwe, katika mkutano wa dharura kujadili namna ya kukabiliana na mzozo unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu ya Tanzania, Sharifa Nyanga, Rais Samia Suluhu Hassan anashiriki mkutano huo. Mkutano huu unafuatia kikao cha dharura cha Utatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ Troika) pamoja na nchi zinazochangia askari katika Misheni ya SADC nchini DRC (SAMIDRC), kilichofanyika Januari 28, 2025, chini ya uenyekiti wa Rais Samia.

Mkutano huu unafanyika wakati maelfu ya wakazi wa DRC wakiendelea kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi yanayoendeshwa na waasi wa M23, kundi linalozidi kutwaa maeneo muhimu ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Sekretarieti ya SADC, kikao hiki cha dharura cha wakuu wa nchi na serikali kitaongozwa na Mwenyekiti wa SADC, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, na kitanguliwa na vikao vya Kamati ya Kudumu ya Viongozi Wakuu wa SADC pamoja na Baraza la Mawaziri la SADC.

SADC, jumuiya ya kikanda inayojumuisha nchi wanachama 16, ikiwemo DRC, imekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kurejesha amani na utulivu nchini humo. Wanachama wengine wa SADC ni Angola, Botswana, Comoro, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia, na Zimbabwe.

Mkutano huu unafuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa na ujumbe wa kulinda amani wa SADC Mashariki mwa DRC, hali iliyosababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Siku ya Jumatatu, Rais Mnangagwa alilaani mashambulizi hayo na kusisitiza kuwa SADC itachukua hatua za haraka kukabiliana na kuzorota kwa hali ya usalama na kibinadamu nchini DRC. Mnamo Novemba 2024, SADC iliongeza muda wa ujumbe wake wa kulinda amani nchini humo kwa mwaka mmoja zaidi, kutokana na kuendelea kwa mapigano kati ya jeshi la DRC na makundi yenye silaha, hali iliyosababisha zaidi ya watu 400,000 kukimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa 2025.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amezungumza kwa njia ya simu na marais wa DRC na Rwanda kujadili mzozo huo unaozidi kuwa mbaya. Hadi sasa, waasi wa M23 wanadhibiti sehemu za Goma, mji mkubwa zaidi Mashariki mwa DRC, huku Rwanda ikiendelea kukanusha madai kuwa inawaunga mkono waasi hao.