ZRA yawatua wananchi ndoo kichwani

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 10:19 AM Dec 28 2024
Waziri wa Nchi Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya akimtwisha ndoo ya maji Asha Makame mkazi wa  Kiungani Donge baada ya wananchi hao kujengewa kisima hicho na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Picha:Mtandao
Waziri wa Nchi Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya akimtwisha ndoo ya maji Asha Makame mkazi wa Kiungani Donge baada ya wananchi hao kujengewa kisima hicho na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Mkoa wa Kaskazini Unguja.

MAMLAKA ya Mapato Zanzibar (ZRA) imewatua ndoo kichwani wananchi wa kijiji cha Donde Kiungani kwa kuwachimbia kisima kwa ajili ya kupata huduma ya maji safi na salama, ikiwa ni sehemu ya mwezi wa shukrani kwa walipakodi.

Wakizungumza katika hafla ya ufunguzi wa kisima hicho iliyofanyika kijijini hapo,  wananchi wa kijiji hicho walisema uwapo wa kisima hicho ni faraja kwao kwa sababu wameondokana na changamoto ya kutafuta maji kwa umbali mrefu huku kinamama wakiwa waathirika wakubwa. 

Fatma Khamis, mmoja wa wananchi hao, alisema kabla ya uwapo wa kisima hicho walikabiliwa na changamoto ya huduma ya maji jambo ambalo liliwarudisha nyuma katika kushiriki harakati mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“Maji ndiyo kila kitu katika maisha ya binadamu. Nilikuwa  nikiamka asubuhi tu nawaza kwenda kutafuta maji hali ambayo ilinigharimu sana kwa sababu muda mwingi naupoteza huko bila ya kushiki kikamilifu katika shughuli zangu za kiuchumi,” aisema Fatma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, itahakikisha inaendelea kufikisha maendeleo katika maeneo yote ya Unguja na Pemba hususan huduma za maji, umeme, afya na elimu ili kuwawezesha wananchi kunufaika na maendeleo hayo.

Alisema maendeleo yote ambayo yanafanyika hivi sasa yanatokana na kodi zinatokana na wananchi wenyewe, hivyo aliwataka kushirikiana na serikali kudai risiti za kielektroniki na kuiwezesha serikali kufanya mambo makubwa zaidi.

Pia alisema zinasaidia kuleta maendeleo kwa nchi na wakiona barabara, maji, umeme na miundombinu mingine, wajue ni kodi za wananchi wenyewe ambazo wanailipia anapofanya ununuzi wa bidhaa mbalimbali. 

Alisema serikali inafanya jitihada kubwa za usambazaji wa maji safi na salama lakini kuna baadhi ya maeneo ya kilimo hayajafikiwa na miundombinu hiyo, hivyo kuna haja ya kurejesha jambo hilo kwa wananchi wa kijiji hicho.

Waziri Saada aliitaka ZRA kuangalia namna ya kuendelea kusaidia maeneo mengine ambayo yanahitaji miundombinu hiyo.

“Wananchi wa Donge mtambue kuwa kisima hiki ni kodi zenu wenyewe ambazo zinamuwezesha mwananchi kudai risiti za kielektroniki hivyo tuendelee kulipa kodi kwa kudai risiti kila mnapofanya manunuzi,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya ZRA, Prof. Hamed Rashid Hikmany, aliwataka wananchi kuendelea kuisaidia serikali kupata mapato ili kumwezesha Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi aendelee kufanya maendeleo makubwa kwa kushajihishana kudai risiti za kielektroniki.

Pia aliwataka wafanyabiashara kuwapa risiti wananchi ili kuwa waaminifu na kodi inaifikia serikalini ili kutekeleza upatikanaji wa huduma mbalimbali muhimu kwa maslahi ya taifa.

Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohammed, alisema mamlaka hiyo imepewa jukumu la kumsaidia Rais kukusanya mapato ya serikali ambayo yanatoka kwa wananchi.

Alisema kodi hiyo inakwenda moja kwa moja katika maendeleo, hivyo ni vyema kudai risiti za kielektroniki ili nchi iendelee kupiga hatua za kimaendeleo.

Kuhusu mwezi wa shukran na furaha kwa walipakodi, alisema ZRA imejipanga kila mwaka kwa mwezi huo  kutoa shukran kwa walipakodi ikiwamo kufikisha elimu kwa wananchi na kurudisha ihsani kwa walipakodi wao.