Ukusanyaji kodi kwa mabavu kwamchefua RC

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:38 AM Jun 26 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.
Picha: Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amewaonya watumishi ambao wamekuwa wakikusanya mapato waache kutumia nguvu.

Alitoa onyo hilo juzi wakati akitoa salamu za viongozi wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kilicholenga kujadili utekelezaji wa maagizo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Alisema ukusanyaji mapato ni nguzo ya halmashauri, kwamba itatekeleza shughuli zake kwa ufanisi, isije tumika nguvu kubwa wakati wa ukusanyaji wa mapato, bali wananchi wapewe elimu na kulipa kwa utaratibu.

“Tuzingatie ubinadamu wakati wa ukusanyaji mapato na siyo kutumia nguvu kubwa, elimu itolewe kwanza juu ya umuhimu wa kulipa mapato na wale ambao watakaidi fuateni taratibu ikiwamo kushirikisha polisi,"alisema Macha.

Aidha, aliwasisitiza wataalamu kubuni vyanzo vipya vya mapato, pamoja na madiwani kuhamasisha wananchi kulipa mapato kupitia kwenye mikutano yao, huku akiipongeza Halmashauri ya Kishapu kwa kupata hati safi kutokana na kujibu hoja za CAG na kutoa angalizo wasije wakalewa sifa bali waendelee kuchapa kazi kwa bidii na kufuata taratibu zote za utumishi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, alisema zamani halmashauri hiyo ilikuwa kwenye nafasi ya 10 bora ya halmashauri hapa nchini yenye hoja nyingi za CAG.