WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Tanzania inathamini mchango mkubwa wa Marekani katika maendeleo ya nchi kupitia miradi na programu mbalimbali zinazofadhiliwa na nchi hiyo.
Miongoni mwa programu hizo ni mkataba wa msaada wa dola za Marekani bilioni 1.14, uliotiwa saini hivi karibuni kwa ajili kuendeleza sekta mbalimbali.
Dk. Nchemba aliyasema hayo jijini hapa jana wakati akiagana na Balozi wa Marekani aliyemaliza muda wake wa uwakilishi Tanzania, Michael Battle. Waziri na balozi huyo walitumia fursa hiyo kujadili maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani hususan katika biashara na uwekezaji.
“Ninashukuru kwa msaada wa Dola za Marekani bilioni 1.14 uliotolewa na taasisi za Marekani kupitia programu ya Development Objectives Agreement (DOAG), unaoonesha namna Marekani inavyochangia maendeleo ya nchi yetu.
“Fedha hizo zitaelekezwa kwenye sekta za afya, elimu, kukuza uchumi na utawala bora, hivyo kuchangia Agenda ya Dira ya Taifa ya 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26,” alisema Dk. Nchemba.
Dk. Nchemba alirejea pia shukrani zake kwa Marekani kwa kuipa nafasi Tanzania ya kuboresha masuala kadhaa kupitia Mradi wa Millenium Challenge Corporation (MCC), ili nchi irejee kwenye mpango mkuu wa maendeleo na kwamba serikali imeimarisha kwa kiasi kikubwa misingi ya demokrasia, haki za binadamu, utawala bora pamoja na maendeleo ya nchi.
Balozi Battle alisema Marekani na Tanzania ni washirika wa muda mrefu wa maendeleo na kwamba uhusiano huo umeendelea kudumishwa na kuimarishwa hadi sasa.
Battle aliyeambatana na Naibu wake, Andrew Lentz, alisema ushirikiano huo unatarajia kuchukua mwelekeo mpya kwa kuhimiza zaidi biashara na uwekezaji kwa faida ya pande zote mbili hususan kwa kutumia ukanda wa kibiashara wa Bahari ya Hindi pamoja na uwepo wa fursa ya gesi (LNG).
Aidha, alisema Marekani inaandaa mpango mpya wa kutumia Sheria ya ukuaji wa fursa Afrika (AGOA) unaolenga kukuza masoko na biashara ndani na nje ya Marekani, ambapo mwelekeo utakuwa ni ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi na nchi (bilateral) badala ya Marekani na mataifa mengi kwa pamoja (Multilateral).
Mazungumzo ya kuagana na Balozi Battle, yalimhusisha pia Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Amina Khamisi Shaaban, viongozi waandamizi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED