Bandari Dar yapokea meli ya kontena 4,000

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:27 PM Dec 09 2024
Hafla ya kupokea meli kubwa ya mizigo kutoka China kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Picha:Mpigapicha Wetu
Hafla ya kupokea meli kubwa ya mizigo kutoka China kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeendelea kupokea meli kubwa za mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ikitokea China yenye uwezo wa kusafirisha zaidi ya kontena 4,000.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, kwenye hafla fupi ya kuipokea meli kubwa ya mizigo inayoitwa EverGreen Line Group, Meneja wa Zimamoto na Usalama wa TPA, Mussa Biboze amesema uwekezaji na uboreshwaji mkubwa uliofanywa katika bandari hiyo umekuwa ukiwavutia wawekezaji pamoja na mawakala mbalimbali wa kampuni za meli kuleta meli zao kupitia bandari hiyo.

Amesema  kuwa uwekezaji na uboreshwaji mkubwa uliofanywa katika bandari hiyo  umekuwa ukiwavutia  wawekezaji pamoja na mawakala mbalimbali wa makampuni za meli kuleta meli zao kupitia Bandari hiyo.

“Uwekezaji mkubwa  wa miundombinu uliofanywa na  Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TPA katika  Bandari ya  Dar es Salaam umechangia   kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kiutendaji na hivyo kuvutia kampuni kama  EverGreen Line Group kuleta meli yake kwenye bandari yetu,” amesema Biboze.

Amesema miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja uwepo wa kamera za ulinzi na usalama za kutosha katika eneo lote la Bandari pamoja na kuongezeka kwa krane ambazo zinasaidia kushusha na kupakia kontena ndani ya muda mfupi sana, hivyo kufanya meli isitumie muda mrefu kukaa  bandarini tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Amesema  mara ya mwisho kampuni hiyo kuitumia bandari ya Dar es Salaam ilikuwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, lakini wamerudi tena baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na wawekezaji wakiwemo  DP World na  Adan International Ports Holding .

1

‘’Napenda kukiri kuwa kampuni hii zinazosimamia gati hizi yameongeza tija kwa Serikali pamoja na kuongeza mapato, lakini pia kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaotumia bandari ya Dar es salaam’’ amesema  Biboze

Biboze amesema ujio wa meli kama hiyo  utaongeza mapato kwa TPA na TRA, huku ukitoa fursa kwa madereva wengi zaidi ambao watahitajika  kwa ajili ya kusafirisha mizigo iliyopo ndani ya makontena hayo.

Naye Meneja wa Kampuni ya EverGreen Line group Tawi la Tanzania,  Mohamed Lotfy  amesema hapo awali walikuwa wanaleta mizigo kupitia meli  ndogo, lakini hivi sasa wameamua kuja na meli kubwa na hiyo yote ni kutokana na maboresho makubwa  katika utoaji huduma yaliyofanyika katika bandari hiyo.

‘’Utafiti tulioufanya umetupa nguvu ya kuleta meli yetu  kubwa  ambayo ina uwezo wa kubeba makontena elfu nne na  tutakuwa na safari moja kila mwezi na baadae tutakuwa na safari mbili kwa mwezi ili tuweze kuleta mizigo zaidi”, amesema Lotfy.
2

Naye Meneja Kitengo cha Biashara na Uhusiano wa Tanzania East Africa Gateway Terminal Ltd,  Donald Talawa amesema ni mafanikio makubwa kupata meli kama hiyo yenye uwezo wa kuchukua kontena nyingi  zaidi kwa wakati mmoja.

‘’Sisi tuko tayari kuipokea na kuihudumia meli hii ambayo ni mpya na ya kisasa ambayo imekuja moja kwa moja kutoka nchini China napenda nikiri kwamba maboresho yaliyofanywa hapa Bandarini yanaruhusu aina ya meli kama hizi kufika kwa sababu ya kuongezwa kwa kina cha bandari’’ ameeleza  Talawa.

Hafla hiyo ya upokeaji wa meli hiyo pia ilihudhuriwa na Meneja Udhibiti wa Huduma za Meli kutoka katika Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC),  Fatma Masenene .

Fatma  amesema ujio wa meli hiyo ni neema kwa Serikali kwa sababu inapata mapato, wamiliki wa bandari kavu, na wafanyabiashara wa bidhaa ndogo ndogo kama vile wa vyakula na maji na hata watu wa usafi watafaidika pia.
3