SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, tangu ilipoingia madarakani mwaka 2021, imekuwa ikihimiza maendeleo ya sekta ya utalii kwa kutangaza vivutio vilivyoko ili kuwavutia watalii wengi zaidi kuingia na kuchangia pato la taifa.
Katika kutimiza azma hiyo, Rais Samia alicheza filamu ya The Royal Tour ambayo imeonyesha vivutio mbalimbali kama vile mbuga za wanyama, magofu ya kale na fukwe zilizoko katika pwani ya Bahari ya Hindi na maziwa mbalimbali. Sambamba na filamu hiyo, serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta hiyo ambayo yamesababisha wageni kuongezeka na kutembelea mbuga za wanyama na maeneo ya kihistoria na pwani visiwani Zanzibar.
Kwa kuonyesha hilo, wakati akimwapisha Mkuu wa Mkoa wa sasa wa Arusha, Paul Makonda, Rais alimwagiza kiongozi huyo kuwa ana jukumu kubwa la kuendeleza sekta hiyo ikizingatiwa kuwa mkoa huo ni kitovu cha utalii.
Bila kusita, Makonda alianza kutekeleza agizo hilo, ikiwamo kuomba ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa wawekezaji wa visiwa hivyo, kuipa Arusha kipaumbele katika ujenzi wa hoteli pia watalii kuanza Zanzibar na baadaye kutembelea mkoa huo au vinginevyo kadiri ya ratiba zao zitakavyokuwa.
Ombi hilo lilikubaliwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuwa ni wazo zuri na linalenga kuendeleza sekta hiyo na kuahidi kuwa serikali yake itazungumza na wawekezaji ili kupanua fursa za uwekezaji pamoja na kampuni za utalii visiwani humo kupanga mipango itakayowezesha watalii kufika Zanzibar na Arusha.
Pamoja na nia njema ya serikali katika kukuza sekta hiyo, kumekuwa na vikwazo mbalimbali ambavyo vinasababisha usumbufu kwa watalii na hata kuiweka nchi katika taswira hasi kimataifa, hivyo kuwafanya wasirudi tena au kuwakatisha tamaa wengine wenye nia ya kufanya hivyo.
Moja ya vikwazo hivyo ni ukaguzi wa mara kwa mara wa watalii wakiwa kwenye magari ama wanapotoka uwanja wa ndege au maeneo ya mipakani wakati wanapoingia kwenye miji ya utalii, hususani Zanzibar.
Kutokana na kuwapo kwa kikwazo hicho, Makonda ameagiza polisi kuacha kusimamisha magari ya watalii yanayoingia katika jiji la Arusha kuanzia Julai Mosi, mwaka huu na kusisitiza kuwa magari yanapoingia Arusha, yanakuwa tayari yameshakaguliwa katika mipaka na viwanja vya ndege, hivyo kukagua yakiwa ndani ya jiji ni kusababisha usumbufu kwa watalii.
Akizungumza jana katika maonyesho ya Karibu Kili Fair (KKF) yanayofanyika katika viwanja vya Magereza Kisongo, mkoani Arusha, yanayojumuisha zaidi ya kampuni 700 za kimataifa kutoka zaidi ya nchi 50, alisema watalii wanaingia nchini na kuingiza fedha, hivyo kuwakagua mara kwa mara ni kuwasababishia kero ambazo zina athari hasi kwa maendeleo ya sekta na taifa kwa jumla.
Hatua ya kuzuia ukaguzi wa watalii ndani ya jiji la Arusha ni ya kupongezwa kwa kuwa kilio hicho kimekuwa cha muda mrefu na kwamba katika baadhi ya maeneo kimekuwa kikiwafanya watalii waone adha hata wakati mwingine wamekuwa wakiombwa rushwa na baadhi ya askari polisi.
Ni dhahiri kwamba kuondolewa kwa kikwazo hicho kitawafanya watalii kuondokana na usumbufu waliokuwa wakiupata awali na sasa hatua hiyo itawezesha Tanzania kupata sifa njema itakayosaidia watalii zaidi kuingia nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED