Yanga yatanguliza mguu mmoja makundi CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:20 AM Sep 15 2024
news
Picha: Yanga
Yanga yatanguliza mguu mmoja makundi CAF

BAO pekee lililofungwa na straika raia wa Zimbabwe, Prince Dube, limeiweka Yanga katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya makundi, Ligi ya Mabingwa Afrika, ushindi wa 1-0 dhidi ya mwenyeji CBE ya nchini Ethiopia.

Hata hivyo, licha ya Yanga kuibuka na ushindi huo, Kocha wao Miguel Gamondi ameonesha kutofurahishwa na safu yake ya ushambuliaji kukosa magoli mengi kwenye mchezo huo.

Baada ya mchezo Gamondi alisema walistahili kuondoka na ushindi wa idadi goli zaidi ya moja lakini hawakufanikiwa kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi.

"Nimefurahi tumepata ushindi, lakini sijaridhishwa na namna tulivyopoteza nafasi nyingi, tulistahili ushindi mkubwa zaidi, tutalifanyia kazi suala hili," alisema Gamondi.

Katika mchezo huo wa jana mkondo wa kwanza, hatua ya kwanza ya ligi hiyo uliochezwa saa 9:00 alasiri kwa saa za Tanzania, Uwanja wa Abebe Bikila, jijini Addis Ababa, Yanga ingeweza kuibuka na ushindi wa mabao mengi kutokana na wachezaji wake, hasa Dube kukosa mabao kadha ya wazi katika namna iliyowaacha midomo wazi mashabiki wengi.

Kwa ushindi huo, Yanga inatakiwa kupata ushindi au sare yoyote nyumbani, Septemba 20, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ili itinge hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo kama ilivyofanya msimu uliopita.

Dakika ya pili tu Yanga walianza kubisha hodi langoni mwa wenyeji wao, na Dube alikosa bao lililookolewa na kipa Firew Getahun Alemayehu.

Dakika moja baadaye CBE ilijibu shambulizi hilo kupitia kwa mchezaji wake Adis Gebal, ambaye aliwatoka walinzi wa Yanga na kuachia shuti lililowababatiza mabeki, mpira ukarudi na kumkuta Fuad Abdul ambaye alipiga shuti lingine lililodakwa vyema na kipa Djigui Diarra.

Dube aliendelea kukosa mabao, kwani dakika ya 12, aliunganisha kwa mguu wa kushoto krosi iliyotoka kwa Pacome Zouzoua, na mpira ulionekana kama unaingia wavuni, lakini kwa mshangao wa wengi uligonga nguzo ya pembeni na kurejea uwanjani, kabla ya mabeki wa CBE kuuondosha kwenye hatari.

Dakika sita baadaye nusura Yanga iandike bao, baada ya mpira wa kona uliookolewa na mabeki kumkuta Pacome akiwa kwenye eneo zuri, aliachia mkwaju mkali wa chinichini ambao ulitoka nje kidogo ya lango na kumfanya kipa, Alemayehu, kuanza kufokea mabeki wake kwa uzembe.

Ilikuwa ni zamu ya wenyeji kukosa bao dakika ya 30, baada ya kufanya shambulizi kali lililomkuta Omari Bashiru, ambaye shuti lake lilipaa juu ya lango.

Akiwa amebaki yeye na kipa, Dube kwa mara nyingine alikosa bao dakika ya 40  na kumkasirisha kocha Gamondi ambaye alionekana kufoka na kurusha mikono juu kwa hasira.

Shambulizi hilo lilianza kwa mpira uliorudishwa kimakosa na mmoja wa mabeki wa CBE na kumkuta Dube akiwa hajakabwa, akavuta hatua mbili na kumchagua kipa, akiwa hatua takriban sita tu kutoka langoni, mpira wake ukatoka nje.

Baada ya kosakosa nyingi, hatimaye Dube alisawazisha makosa yake alipoukwamisha mpira wavuni sekunde chache kabla ya mapumziko, alipomalizia vizuri pasi kutoka kwa Stephane Aziz Ki.

Kipindi cha pili kwa nyakati tofauti Yanga ilifanya mabadiliko, mwanzoni kabisa ikiwatoa Aziz Ki na Dube na nafasi zao kuchukuliwa na Clatous Chama na Clement Mzize, baadaye wakaingia tena Yao Koassi na Duke Abuya kuchukua nafasi za Mudathir Yahaya na Maxi Nzengeli, na dakika tano kabla ya mechi kumalizika aliingia Jean Baleke akipishana na Pacome.

Kabla ya kutoka, Mudathir nusura afunge bao dakika ya 70 baada ya shuti lake kali kuwababatiza mabeki na mpira ukarejea kwa Boka ambaye alipiga krosi iliyounganishwa vibaya na Mzize, ukatoka nje.

Mzize akiwa hatua mnne tu kutoka langoni, alipaisha mpira akiwa peke yake dakika ya 42, baada ya makosa ya walinzi wa CBE waliompa muda wa kuuweka kifuani na kugeuka.

Ilikuwa ni rahisi zaidi kupata bao kuliko kukosa kama alivyofanya Chama dakika za majeruhi, alipowekewa krosi nzuri na Mzize lakini akiwa kwenye nafasi ya kufunga aliunganisha kwa mguu wa kushoto mpira ulionda nje kidogo ya goli.

Yanga inarejea nchini leo kuwasubiri Waethiopia kwa ajili ya mchezo wa marudiano.