Yanga yasaka kiungo mpya

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:35 AM Oct 04 2024
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi

BAADA ya Simba kumsajili winga, Elie Mpanzu, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga nao wako katika mchakato wa kunasa saini ya kiungo mkabaji mpya, Charve Onoya, kutoka AS Maniema ya nchini humo.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema mchezaji huyo ni mmoja ya watakaovaa uzi wa kijani na njano kipindi cha dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba, mwaka huu na Januari, mwakani.

Chanzo chetu kilisema Yanga inataka huduma ya mchezaji hiyo kwa ajili ya kuimarisha eneo lao la kiungo, ambalo kwa sasa linaongozwa na Mganda Khalid Aucho na Aziz Andambwile.

Kiungo huyo nusura ajiunge na Yanga mwanzoni mwa msimu huu, lakini dili lilifeli, na safari hii mabosi wa klabu hiyo wamerejea kwa nguvu zote.

"Kwa sasa tegemeo ni Aucho, na anaonekana amechoka kutokana na kucheza michezo mingi, anahitaji msaidizi, Mudathir yeye anapewa kazi ya kwenda kushambulia mianya inayoachwa na wapinzani, mara chache anakuja kumsaidia.

Andambwile bado hana uzoefu, tuna michuano mingi migumu ya kimataifa, kwa hiyo lazina tupate kiungo mkabaji mzuri na mwenye uzoefu, tumeangukia kwa huyo jamaa Mkongomani," kilisema chanzo kutoka Yanga.

Chanzo hicho kiliongeza upatikanaji wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, umechangiwa zaidi ya kiungo mshambuliaji, Maxi Nzengeli ambaye anatajwa ni rafiki yake na amekuwa akimshawishi mara kwa mara kutua Jangwani.

"Mahesabu ya Yanga ni huyu ndiyo atakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa, na kama kuna wengine basi watafuata," alisema mtoa taarifa.

Habari zaidi zinasema Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameonekana kuridhishwa na viungo washambuliaji, mastraika na mawinga alionao, lakini bado haridhishwi na eneo la kiungo mkabaji.

Kwa sababu hiyo, huenda mchezaji hiyo akasajiliwa kuchukua nafasi ya Jean Baleke, ambaye ameonekana hana namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Taarifa zaidi zinadai huenda Baleke  akapelekwa kwa mkopo Singida Black Stars ili nafasi yake ichukuliwe na kiungo huyo mpya.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kwa sasa si wakati wa usajili, hivyo hawezi kueleza chochote kuhusu mchakato huo na badala yake wako kwenye operesheni ya kuhakikisha wanapanda kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Tuko kwenye operesheni ya kuisaka nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi Kuu, nafasi yetu pendwa ni namba moja, hatuna chochote tutakachoongea au kuwaza zaidi ya kwanza tukae kwenye sehemu tulioizoea, namba moja," alisema Kamwe.