Yanga yamkaribisha Hamdi kibabe

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 08:27 AM Feb 06 2025
Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Stephanie Aziz Ki (kushoto), akiwania mpira dhidi ya mchezaji wa KenGold kutoka Mbeya katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana. Yanga ilishinda mabao 6-1
Picha: Yanga SC
Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Stephanie Aziz Ki (kushoto), akiwania mpira dhidi ya mchezaji wa KenGold kutoka Mbeya katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana. Yanga ilishinda mabao 6-1

MABINGWA watetezi, Yanga wamemkaribisha Kocha Mkuu mpya, Miloud Hamdi, kwa kupata ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya KenGold katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana.

Hamdi ametua Yanga akitokea Singida Black Stars ya mkoani Singida, akiwa amerithi mikoba iliyoachwa na Sead Ramovic, aliyeachana na klabu hiyo ya Jangwani baada ya kufanikiwa kupata dau nono kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria.

Kocha huyo mpya wa Yanga jana alikuwa jukwaani akishuhudia timu yake mpya ikipata ushindi mnono dhidi ya KenGold inayoburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini akiandika 'dondo' ambazo huenda akazitumia katika majukumu yake mapya.

Yanga ilitoa taarifa ya kuachana na Ramovic kwa kuelekeza walifikia makubaliano ya pande mbili ya kuvunja mkataba.

Katika mchezo wa jana, Yanga walianza kwa kasi na iliwachukua dakika moja tu kuandika bao la kwanza kupitia kwa Prince Dube aliyepokea pasi safi ndani ya eneo la hatari kutoka kwa Stephanie Aziz Ki.

Kupatikana kwa bao hilo ni kama kuliwavuruga wachezaji wa KenGold ambao walipoteza utulivu na kuipa nafasi  Yanga kufanya mashambulizi yaliyozalisha bao la pili lililofungwa na Clement Mzize ambaye jana alifikisha magoli tisa.

Kengold licha ya kufanya maboresho ya timu yake katika dirisha dogo la usajili walishindwa kabisa kuhimili kasi ya Yanga huku Pacome Zouazoua akiipatia timu yake bao la tatu dakika ya 38 akiunganisha vizuri pasi ya Mzize.

Mpaka mwamuzi anapuliza filimbi ya kumalizika kipindi cha kwanza, Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 4-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza, iliwachukua tena dakika moja mabingwa hao watetezi kuandika bao la tano kupitia kwa Dube na kama straika huyo Mzimbabwe angeweka makini angefunga ‘hat trick’ kama angetumia vizuri pasi safi ya mtokea benchi, Clatous Chama, alipiga pembeni.

Dakika ya 84, Duke Abuya, aliipatia Yanga bao la sita akiunganisha kwa shuti mpira uliotoka kwa Keneth Musonda, ambaye wote waliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi za Mudathir Yahaya na Pacome.

Mshambuliaji wa Kengold, Selemani Rashid, alimshangaza kipa wa Yanga, Djigui Diarra, baada ya kupiga mpira mrefu katikati ya uwanja eneo la kuanzisha mpira na kutinga wavuni baada ya kushindwa  kuokoa hatari hiyo na kufuta ‘clean sheet’ ambayo angeweza kuondoka nayo.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kupanda kileleni mwa msimamo wakifikisha pointi 45 baada ya kucheza michezo 17 lakini wanaweza kushushwa endapo Simba inayoshuka ugenini dhidi ya Fountain Gate itapata ushindi wowote.