Yanga, Simba mawindoni Ligi Kuu Tanzania Bara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:05 AM Feb 22 2026
Stive Barker, Kocha wa Simba (kushoto) pamoja na Pedro Soares, Kocha wa Yanga
Picha: NipasheDigital
Stive Barker, Kocha wa Simba (kushoto) pamoja na Pedro Soares, Kocha wa Yanga

Vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga, leo watashuka katika viwanja tofauti nchini kuendelea na mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu hizo zote zitakuwa ugenini zikicheza mechi zao za viporo ambazo ziliahirishwa huko nyuma kutokana na kushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi kucheza dhidi ya wenyeji Namungo huku Simba ikiwa jijini Dodoma kucheza na Maafande wa Tanzania Prisons.

Namungo itakuwa inamaliza mechi zake za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikifikisha michezo wa 15 wakati kwa upande wa mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga, utakuwa mchezo wanane.

Mabingwa hao wanaingia uwanjani wakiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo wakikusanya pointi zao 22, huku Namungo ikiwa nafasi ya tano, na pointi zake 20.

Ikumbukwe kuwa Coastal Union iliutumia uwanja huo badala ya CCM Mkwakwani kufungiwa.

Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema wamesahau yote yaliyopita, ushindi katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa, na sasa akili na nguvu zote wanazielekeza kusaka ushindi dhidi ya Namungo.

"Tunataka kutetea ubingwa, huwezi kuutetea kama haushinda michezo ya nyumbani na ugenini. Tunakwenda ugenini kucheza na Namungo, nimekitengeneza kikosi kwa ajili ya kushinda mchezo huu," alisema Pedro.

Simba yenyewe itashuka dimbani kuanzia saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kucheza dhidi ya Tanzania Prisons ambayo kwenye msimamo wa Ligi Kuu iko taabani.

Simba inaingia katika mchezo ikitoka kucheza mechi ya kimataifa baada ya kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali licha ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Stade Malien ya Mali.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, Mnyama anashika nafasi ya saba akiwa na pointi 19, huku Prisons ikiwa nafasi ya 14 na pointi zake 12.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Steve Barker, amesema maandalizi yapo vizuri na wachezaji wake wamejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo huo.

"Maandalizi yamekwenda vizuri, najua hautokuwa mchezo rahisi, tumejiandaa kushinda, lakini si kwa kuwadharau wapinzani.

Wakati huohuo, Azam FC leo itashuka kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kucheza dhidi ya wenyeji wao, KMC ambao mwenendo wao kwa sasa ni wa kutia shaka msimu huu.