HATIMA ya Yanga kufuzu hatua ya robo fainali itajulikana leo baada ya mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Yanga inayotamba na msemo wao wa hamasa wa 'gusa, achia twende kwao' leo watakuwa na kazi moja tu ya kugusa kuachia kwenda robo fainali, ikimaanisha ushindi wowote watakaoupata utawavusha kutinga katika hatua hiyo kwa mara ya pili mfululizo.
Kabla ya mchezo wa leo, Yanga imepishana kwa pointi moja na wapinzani wao wenye pointi nane na kushika nafasi ya pili kwenye kundi huku Yanga wakiwa na pointi saba wakishika nafasi ya tatu.
Hii inamaanisha kama Yanga watakubali kipigo au sare yoyote itawapa nafasi MC Alger kuungana na Al Hilal kutinga hatua hiyo huku Yanga na TP Mazembe zikiaga michuano hiyo.
Kuelekea katika mchezo huo wa leo, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, alisema wamejipanga kupata pointi tatu katika mchezo huo ili wafuzu hatua inayofuata.
Alisema kuwa wanatambua mchezo huo ni muhimu kwao, hivyo amewataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono timu yao waweze kufuzu hatua ya robo fainali.
"Kila siku malengo yetu ni kushinda, tumejiandaa vizuri na kila mchezaji na morali ya juu kuhakikisha tunakwenda kutimiza malengo yao," alisema Ramaovic.
Alisema anafahamu mchezo utakuwa mgumu kutokana na aina na wapinzani wanaokutana nao, lakini wana faida ya kucheza mbele ya mashabiki wao ambao anaamini watajitokeza kwa wingi uwanjani.
"Tutacheza kwa nidhamu kubwa sana, tuna mbinu zetu tutakazozitumia ambazo naamini zitatupa ushindi, hatutawapa nafasi ya kuutawala mchezo, kwa sababu hiyo itakuwa tatizo kwetu," alisema Ramovic.
Kwa upande wake, Nahodha wa Yanga, Dickson Job alisema wao kama wachezaji wapo tayari kwa mchezo wa kesho (leo) na kusema wanahitaji matokeo mazuri ili wafanikiwe kuingia hatua ya robo fainali.
“Tunaelewa umuhimu wa mchezo wa kesho (leo), tunatambua ukifanya kosa moja itakuwa tatizo kubwa, kumaliza mechi nyumbani ni faida kwa sababu tunakuwa karibu na mashabiki wetu, tutapambana kuhakikisha tunashinda mchezo huu kwa sababu kinyume cha hapo tunaondolewa kwenye mashindano, mashabiki waje watuunge mkono na kutupa sapoti yao,” alisema Job.
Aidha, Kocha Mkuu wa MC Alger, Khaled Benyahya, alisema mchezo huo ni muhimu na hivyo wamejipanga kukabiliana na Yanga licha ya kuwa ugenini.
Alisema japokuwa Jiji la Dar es Salaam lina joto kuliko Algeria hana wasiwasi kwani wapo tayari kucheza kwenye mazingira yoyote.
Alisema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kiufundi kutokana na umuhimu kwa kila timu kusaka nafasi ya kuingia robo fainali.
"Kampeni yetu ilianza hatua za awali na kufanikiwa kupata matokeo mazuri katika michezo yetu tuliyoicheza hivyo tunaamini kesho (leo) tutapata matokeo mazuri," alisema Benyahya.
Kwa upande wake, mchezaji MC Alger, Zakaria Draoui alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwa pande zote.
"Sisi tunafahamu umuhimu wa mechi hii, lazima tucheze kwa maamuzi ambayo yatatusaidia kuingia hatua inayofuata," alisema Draoui.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED