BAADA ya miaka 23 kupita, Yanga leo wanakutana kwa mara ya pili na mabingwa wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo safari hii wanakutana katika hatua ya robo fainali kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana kwenye hatua ya awali mwaka 2001 ya michuano hiyo ambapo katika mchezo wa kwanza Mamelodi Sundowns ilishinda kwa mabao 3-2 wakati mchezo wa marudiano uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Yanga ililazimishwa sare ya mabao 3-3.
Yanga leo wana nafasi ya kulipiza kisasi kwa wasauzi hao kwenye mchezo utakaoanza saa 3:00 usiku.
Kuelekea kwenye mchezo wa leo hatua ya makundi, Yanga wamefikia hatua hiyo baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi D la michuano hiyo nyuma ya vinara Al Ahly ambao jana walicheza na Simba kwenye hatua hiyo ya robo fainali.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ambaye amewahi kuwafundisha wasauzi hao mwaka 2006, amesema kila kitu kipo sawa na kazi iliyobaki na wachezaji wake kutimiza yake aliyowaelekeza kwenye uwanja wa mazoezi.
Gamondi alisema mchezo wa leo ni mzuri na mkubwa na lazima watumie vizuri faida ya kucheza uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wao.
“Tupo tayari kwa mchezo wa kesho (leo), ni mchezo mgumu kutokana na aina ya wapinzani wetu lakini tumejipanga vizuri na tumejiandaa kukabiliana nao, kitu muhimu kwetu ni kupata ushindi," alisema Gamondi.
Aidha, amesema licha ya kuwa na majeruhi watatu kwenye kikosi chake Khalid Aucho, Yao na Kibwana Shomari pamoja na kuchelewa kujiunga na timu kwa nyota wake wawili Aziz Ki na Djigui Diarra waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa bado watapambana kuhakikisha wanapata ushindi.
"Diarra na Aucho wamejiunga na timu jana (juzi) asubuhi na watakuwepo uwanjani leo, kukosekana kwa Aucho na Yao naamini wachezaji watakaopewa jukumu watafanya kazi vizuri kwa ajili ya timu na watanzania," alisema Gamondi.
Alisema anafahamu wana michezo miwili dhidi ya Masandawana hao, lakini kwanza anauangalia mchezo wa leo kabla ya kuanza kuipigia hesabu mchezo wamarudiano utakaochezwa Afrika Kusini Aprili 5.
"Matokeo ya mchezo wa leo yatatupa picha ni kazi kubwa kiasi gani tutakuwa nayo kwenye mchezo wa marudiano, kama kocha nataka mchezo tuumalize hapa Dar es Salaam," alisema Gamondi.
Hata hivyo mchezo wa leo utakuwa na upinzani mkubwa kutokana na kikosi cha Mamelodi chini ya kocha wake Rhulani Mokwena kuwa na kiu ya kurudia mara ya pili mafanikio yao ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.
Mamelodi ikiwa chini ya kocha Pitso Mosimane ilifanikiwa kutwaa ubingwa huomwaka 2016 na msimu uliopita ilicheza hatua ya nusu fainali na kuondolewa na Wydad Casablanca.
Mlinda mlango namba moja wa timu ya taifa ya Afrika Kusini 'Bafanabafana', Ronwen Williams leo atakuwa muhimili muhimu wa Mamelodi kuzuia mipira ya washambuliaji wa Yanga.
Aidha, kurejea kwa nahodha wao Themba Zwane kunatarajia kuongeza makali yao kwenye safu ya kiungo kutokana na ubora wa nyota huyo aliyefanya vizuri akiwa na Bafanabafana kwenye fainali za Afcon zilizofanyika hivi karibuini Ivory Coast.
Kuelekea mchezo huo, Kocha Mokwena aliweka wazi kuwa wanaiheshimu Yanga kwa kuwa ni miongoni mwa timu kubwa Tanzania na Afrika hivyo wamechukua tahadhari zote.
“Niliwaangalia katika mchezo dhidi ya Simba na Azam FC, pia kocha wao amewahi kufundisha Mamelodi Sundowns, haitakuwa mechi tahisi lakini tumefanya maandalizi mazuri na tupo tayari kwa mchezo wetu dhidi ya Yanga,” alisema Mokwena.
Aliongeza kuwa malengo yake makubwa ni kumaliza mchezo hapa Dar es salaam japo anafahamu hilo ni gumu kutokana na ubora wa wapinzani wao.
Alisema atacheza kwa tahadhari mechi ya leo kutokana na ubora na ugumu wa Yangahasa afu yao ya ulinzi huku akiwataja Ibrahim Bacca na Dickson Job kuwa ni mabeki wazuri.
“Mbali na safu ya ulinzi lakini kiungo kuna Khali Aucho, Yao Koussi, Joyce Lomalisa, Stephen Aziz Ki na safu ya ushambuliaji kuna Guede, Clement Mzize na Kennedy Musonda najua kila mmoja na uwezo wake, hatuwaogopi bali tunawaheshimu Yanga,” alisema Mokwena.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED