Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo wana kibarua ‘kizito’ cha kuhakikisha wanatinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakapowakaribisha JS Kabylie kutoka Algeria kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mechi hiyo ya mwisho ya hatua ya makundi itachezwa kuanzia saa 1:00 usiku sawa na mchezo mwingine wa Kundi B utakaowakutanisha Al Ahly ya Misri dhidi ya AS FAR Rabat kutoka Morocco.
Yanga itaingia na kazi moja tu ya kuhakikisha inashinda mabao kuanzia matatu kwenda mbele, lakini ikiomba wenyeji, Al Ahly wawafunge AS FAR.
Ili Yanga ifuzu inatakiwa ifunge idadi hiyo ya mabao na Al Ahly ishinde, kinyume cha hapo itakuwa imetolewa kwenye hatua ya makundi kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Ni kwa sababu Yanga ina pointi tano, huku AS FAR ikiwa na pointi nane, hivyo sare yoyote itawafanya wawakilishi wa Morocco kufikisha pointi tisa ambazo Yanga haiwezi kufikia hata wakishinda mchezo huo.
Idadi ya mabao inayotakiwa Yanga kushinda imekuwa kubwa kutokana na kuzidiwa idadi ya mabao ya kufunga na fukungwa.
Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema wapo tayari kwa mchezo huo ambao utakuwa mgumu na unaohitaji mbinu zaidi.
"Kwa sasa tunahitaji ushindi tu. Kwa maana hiyo tunahitaji tushambulie zaidi, tunahitaji kutengeneza nafasi zaidi na kuzitumia pia ili tupate tunachokihitaji, si ushindi tu bali idadi ya mabao tunayohitaji kufunga," amesema kocha huyo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED