Wawekezaji nchini watakiwa kuchangamkia AFCON 2027

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:52 AM Apr 17 2024
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa.

WIZARA ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, imewataka wawekezaji wa hapa nchini kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazopatikana kutokana na Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwaka 2027 (AFCON 2027).

Tanzania, Kenya na Uganda watakuwa wenyeji wa fainali za AFCON 2027.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, katika ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji kati ya Wadau wa Sekta ya Michezo na Utalii kuelekea AFCON 2027, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema katika michezo kuna fursa kubwa na huu ni wakati wa wawekezaji wa ndani kujitokeza.

Msigwa alisema katika kuhakikisha huduma mbalimbali zinapatikana kwa kiwango bora, serikali imetenga viwanja 14 kwa ajili ya ujenzi wa hoteli eneo jirani na utakapojengwa uwanja wa kisasa jijini Arusha.

Alisema pia serikali tayari imeshaanza mchakato wa ujenzi mwingine wa uwanja wa kisasa katika Jiji la Dodoma huku tayati maboresho yakiwa yameshafanyika kwenye Uwanja wa Amaan uliko visiwani Zanzibar na umeshakaguliwa.

Katibu huyo alisema ili kuongeza fursa zaidi kupitia michezo, Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya dunia ya baiskeli ambayo yatafanyika jijini Arusha.

“Kutakuwa na fursa mbalimbali kabla ya AFCON, wakati wa AFCON na baada ya AFCON, wawekezaji wasiogope kuwekeza katika michezo,” alisema Msigwa.

Aliongeza kwa kukipongeza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa kuandaa kongamano hilo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani.

Naye Mkurugenzi wa TIC, Gilead Teri, alisema kituo chake kitasaidia wawekezaji mchakato wa kusajili kampuni, kujisajili na mfumo wa ulipaji kodi, kupata kitambulisho cha taifa na usaidizi wa eneo atakalochagua kama linaendana na uteuzi wake.

Alisema serikali imeweka maofisa wa pamoja ambao watamsaidia mwekezaji kupata leseni na kibali kwa ajili ya kuendesha shughuli anazotaka kufanya na kwamba TIC inapenda kuona asilimia 99 ya wawekezaji wakiwa ni Watanzania.