Mvua yaleta maafa kila kona, watoto saba wafariki

By Christina Haule ,, Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 09:52 AM Apr 30 2024
Maafa kwenye jamii.
PICHA: MAKTABA
Maafa kwenye jamii.

ATHARI za mvua inayoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini zimezidi kuleta maafa ikiwamo watoto saba kufariki dunia wilayani Ulanga, mkoani Morogoro, pamoja na wananchi zaidi ya 4,000 kukosa makazi wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mbunge wa Ulanga, Salim Alaudin, amesema mvua inayonyesha wilayani Ulanga imesababisha athari mbalimbali zikiwamo kaya 70 kukosa makazi, nyumba zaidi ya 259 kuzingirwa na maji, hekari 5,000 za mashamba ya mpunga kuharibiwa.

Amesema watoto saba wamefariki na wakati wa kukabiliana na changamoto hiyo alifanikiwa kuwawekea maturubai wananchi waliokosa makazi wa Kata ya Mbuga, Ilonga na Ketaketa.

“Nimefanikiwa kuwawekea maturubai ya kuishi hapo na familia zao, tumewapa chakula cha awali, bado wanahitaji msaada, sambamba na ugumu wa maisha kwa sasa unatokana na magari ya msaada hayawezi kufika Ulanga, barabara kuanzia Lupilo kupandisha Mwaya haipitiki na vyakula vimepanda bei mara mbili ya awali,”  amesema Hasham. 

Amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kukabiliana na changamoto za mafuriko wanazokumbana nazo tangu mvua ilivyoanza kunyesha.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Edson Wiliamsoli, amesema athari za mvua hiyo ni kubwa ikiwamo kuleta mafuriko ambayo yameharibu pia miundombinu.

Mwenyekiti huyo amezitaja shule zilizofungwa kwa muda ili kulinda uhai wa watoto wanapokwenda na kurudi shule kuwa ni Shule ya Msingi Kivukoni A, Tulizamoyo na Mikochi.      

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Morogoro Alinanuswe Kyamba,  amesema tayari makandarasi wapo kwenye kila wilaya wakishughulikia maeneo korofi yaliyoathiriwa na mvua.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Saida Mahugu,  amesema tayari ameshawasilisha taarifa za uharibifu wa mvua inayoendelea kunyesha.

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye,  amesema wananchi 4,000 wamekosa makazi baada ya nyumba zao kukumbwa na mafuriko wilayani Moshi.

Sumaye, ametoa taarifa hiyo baada ya kupokea misaada ya kibinadamu kutoka kwa mfanyabiashara maarufu na mwanasiasa, Ibrahim Shayo (Ibra Line).

Amesema kwa sasa madhara yaliyoletwa na mvua ni makubwa, kwa kuwa watu hao wana uhitaji wa chakula na malazi kwa maana ya nyumba na magodoro.

“Jumla ya kaya ambazo tumezifanyia tathimni, kupitia kamati za maafa, kuna kaya 1,000 wamepata madhara.

“Wako watu ambao nyumba zao hazikuwa bondeni, lakini zimeingia maji, vyakula na samani zote za ndani zimeharibika. Wito, tuwasaidie ndugu zetu kuwachangia ili tuweze kuwarudisha katika hali ya kawaida ya maisha ya kila siku,”  amesema  Sumaye.

Mfanyabiashara Ibra Line, ameguswa na maafa hayo na kutoa msaada wa magodoro 50, mahindi magunia 10, mchele kilogramu 75, ndizi mikungu 41, sabuni ya jamaa katoni tatu, madaftari makasha matano, taulo za kike katoni tano, kalamu katoni 20 kwa ajili ya wanafunzi waliopoteza vifaa vya shule.

Aidha, amemkabidhi Mkuu huyo wa wilaya, Sh. 700,000 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa Wilaya ya Moshi walioathirika na mafuriko hayo kushonewa sare mpya za shule.