Zitto: Watanzania hawapendi kuwa wanademokrasia

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 01:01 PM Apr 30 2024
KIONGOZI wa zamani wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
PICHA: ACT WAZALENDO
KIONGOZI wa zamani wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

KIONGOZI wa zamani wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema moja ya tatizo linalowatesa Watanzania kwa sasa ni kupenda demokrasia lakini hawataki kuwa wanademokrasia.

Amesema na wale walioko katika madaraka hawafikirii kujenga kizazi kipya cha wanasiasa vijana.

Ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano mkuu wa kidemokrasia na miaka 10 ya kuzaliwa kwa chama hicho, kueleza changamoto kubwa inayokabili Tanzania ni kwamba, wapo watu wanapenda demokrasia lakini hawataki kuwa wanademokrasia.  

Amesema: "Kwa hiyo linapokuja suala la haki zao wako mstari wa mbele lakini wakipata nafasi wao ndiyo wanakuwa wakandamizaji wa wengine. Unaiona hiyo hata watu kabla hawajawa kwenye madaraka.

Ameongeza: "Unakuta mtu akishakuwa na hoja yake, hoja ya mtu mwingine haina maana. Kwa hiyo unajua kabisa huyu siyo mwana demokrasia. Kwa hiyo nadhani tubakie na tujitahidi kuwa wana demokrasia.

Zitto amesema: “...Na la mwisho ni kujenga kizazi cha viongozi wapya. Inawezekana kabisa sisi ambao tumeshahudumu, tumeshakuwa na mamlaka ya kiuongozi labda tumeshafikia mahali ambapo hatubadilishiki tena.

Ameongeza: “Lakini kuna vijana wanaibuka, ni lazima tuwajenge wachukue yale mazuri yetu halafu wayaepuke yale mabaya yetu. Kwa maana ya kuwajenga kuwa wana demokrasia."

Kutokana na uhitaji huo, Zitto,  amesema anaiona ACT-Wazalendo, ikiibua aina mpya ya ujenzi wa siasa za hoja na siyo siasa za ulaghai zinazoendelea kuvuruga taswira ya siasa.

Zitto  amesema: "Na mimi nafurahi tumeanzisha Shadow cabinet (Kamati ya wasemaji wa kisekta). Inaibua wanasiasa wapya kabisa. Tunaleta majina mapya, watu wapya na tunawapa nafasi, tumewaruhusu nendeni angukeni tutawainua mpaka mtakapokomaa."