KOCHA Mkuu wa Tabora United, Anicet Kiazayidi, ameamua kubadilisha ghafla 'programu' ya mazoezi kwa wachezaji wake baada ya kusikia Ligi Kuu Tanzania Bara itarejea tena wiki ya kwanza mwezi Februari badala ya Machi Mosi.
Awali, kikosi hicho ambacho kilikuwa kimerejea kambini, kilikuwa na aina nyingine ya mazoezi, lakini Bodi ya Ligi ilipotangaza kuwa Ligi Kuu itarejea mapema zaidi kuliko mwanzo, kocha huyo ameamua kuzidisha dozi kwa wachezaji wake.
Hilo limebainishwa na Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Khalfan Mbonde, ambaye alisema walianza mazoezi taratibu kwa lengo la kuongeza kasi kadri muda unavyokwenda, lakini baada ya taarifa ya Bodi ya Ligi, kila kitu kimebadilika.
"Tulianza mazoezi, lakini kwa sababu tulijua ligi itarejea mwezi Machi, tulikuwa na aina nyingine ya 'programu', twende kidogo kidogo na kuongeza kasi taratibu kadri muda unavyozidi kwenda juu.
Lakini baada ya kusikia ligi inarejea mapema, 'programu' imebadilika, tumeongeza kasi na dozi kubwa kwa wachezaji ili kuendana na muda, tunaamini mzunguko wa pili tutafanya vizuri zaidi kuliko hata wa kwanza. Mzunguko wa kwanza tulifanya vizuri, lakini kuna vitu tuliona vimepungua, tumekuja kuviongeza kwa ajili ya mzunguko wa pili," alisema kocha huyo.
Kuhusu usajili, alisema tayari wameongeza wachezaji sita kipindi cha dirisha dogo la usajili hivyo kuwataka mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi kwani kikosi kitakuwa bora zaidi kuliko kulivyokuwa mzunguko wa kwanza.
"Tumesajili wachezaji sita, mashabiki wa Tabora United wasiwe na wasiwasi, lengo letu ni lile lile, tukikosa ubingwa na nafasi ya pili, basi tusikose ya tatu au ya nne, yaani msimu ujao tunataka kucheza michuano ya kimataifa," alisema Mbonde.
Baadhi ya wachezaji iliyowasajili ni kiungo mkabaji, Cedric Martial Zemba, raia wa Cameroon aliyekuwa akiichezea klabu ya Touranga ya Morocco, na kipa Jean Noel Amonome, raia wa Gabon, aliyekuwa akiichezea Arta Solra7 ya Djibouti.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED