Uhamiaji FC hawatafanya makosa CAF

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 07:34 AM Jul 13 2024
KOCHA wa timu ya Uhamiaji FC, Abdulsaleh Abdallah.
Picha: Mtandao
KOCHA wa timu ya Uhamiaji FC, Abdulsaleh Abdallah.

KOCHA wa timu ya Uhamiaji FC, Abdulsaleh Abdallah amesema hawataki kufanya makosa katika mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Barani Africa..

Uhamiaji FC itakutana na timu kutoka Libya japo bado hawajaijua timu gani.

Uhamiaji itashuka uwanjani kati ya Agosti 17 na 18 mwaka huu katika uwanja wa Amaan Visiwani hapa.

Akizungumza na gazeti hili Kocha huyo alisema kwa mara ya kwanza timu hiyo inashiriki mashindano hayo makubwa hivyo nia yao kubwa ni kuona wanafanya vizuri katika hatua hiyo ya awali.

Alisema kuanzia nyumbani katika mchezo wao wa kwanza utawapa faida kubwa hasa katika kuwasoma wapinzani  wao.

Alisema kupitia mchezo huo utawapa mbinu ambazo wataenda nazo ugenini  kuhakikisha wanafanikiwa kupata ushindi.

Alisema wanakabiliwa na mchezo mgumu kwa kuwa soka la nchi hiyo limepiga hatua hasa katika mashindano kama hayo.

"Tunakutana na timu ambayo inatoka katika nchi ambayo kila mtu anajua soka la nchi hiyo, licha ya kutoijua timu gani lazima tuwe na maandalizi ya kutosha,"alisema.

Hata hivyo alisema ingawa ni wanageni katika mashindano hayo hiyo haimaanishi kama watashindwa kutimiza lengo la kusonga mbele.