TFF kufanya mkutano mkuu Kahama wiki ijayo

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 06:47 PM Feb 20 2026
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF Azan Mufti akizungumza na vyombo vya habari kuhusu ujio wa mkutamo mkuu wa TFF wilayani Kahama mkoani Shinyanya.
PICHA: SHABAN NJIA
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF Azan Mufti akizungumza na vyombo vya habari kuhusu ujio wa mkutamo mkuu wa TFF wilayani Kahama mkoani Shinyanya.

Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unatarajiwa kufanyika wiki ijayo, tarehe 27 na 28 Februari 2026, katika Wilaya ya Kahama, na utakuwa ni mara ya kwanza shirikisho hilo kufanya mkutano wake wa kawaida katika wilaya hiyo.

Mkutano huo unatarajiwa kuibua fursa za maendeleo ya mpira wa miguu katika Wilaya ya Kahama, pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara na watoa huduma kutokana na ushiriki wa zaidi ya wajumbe 400 kutoka sehemu mbalimbali za nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Azan Mufti, amesema ujio wa mkutano huo ni heshima kubwa kwa wakazi wa Kahama na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla. Amesema mkutano huo utatoa nafasi kwa wadau wa soka kubadilishana mawazo, kujadili changamoto, na kuweka mikakati mipya ya kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu nchini, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa utakaoweza kupokea zaidi ya watu 7,000.

Mufti amewataka wananchi wa Kahama kujitokeza kuupokea mkutano huo kwa moyo wa ushirikiano na kutumia fursa hiyo kiuchumi kwa kutoa huduma mbalimbali kwa wageni watakaofika wilayani humo. Aidha, amewahimiza vijana kushiriki kwa wingi shughuli zinazohusiana na mkutano huo ili kujifunza na kunufaika na uwepo wa viongozi wakuu wa soka nchini.

Ameongeza kuwa Rais wa TFF, Wallace Karia, anatarajiwa kuwasili Kahama Februari 25 kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya mkutano kufanyika rasmi.

Awali mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika Februari 21, lakini ukaahirishwa hadi Februari 28, mwaka huu, huku zaidi ya washiriki 400 wakitarajiwa kushiriki katika mkutano huo muhimu wa soka nchini.