Stars kusaka pointi tatu kwa Zambia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:50 AM Jun 11 2024
news
PHOTO: COURTESY
Taifa Stars players, Simon Msuva (left) and Mudathir Yahaya, fight for the ball during the training session.

TIMU ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars', leo saa 11 kwa saa za nyumbani itashuka Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola, kuvaana na wenyeji wao Zambia, katika mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2026 katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.

Stars inacheza mechi hiyo, ikiwa imetoka kufanya maandalizi yake nchini Indonesia ambapo ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo na kutoka suluhu.

Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, amesema Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro, atawaongoza Watanzania kuishangilia timu hiyo leo.

Alisema kikosi kiko vizuri, huku wachezaji ambao awali hawakuwapo nchini Indonesia wakiwa tayari wamejiunga na wenzao.

"Morali iko juu, wachezaji wote walioitwa kwa ajili ya mechi hii wamefika, wale ambao hawakuwa Indonesia na wengine walioongezwa wote wapo.

Na tunatarajia mheshimiwa Waziri ataungana na timu leo (jana) akitokea Dar es Salaam, timu ilipata mapokezi mazuri kutoka kwa balozi wa hapa, Luteni Jenerali Mathew Mtingule," alisema Wambura.

Alisema kumekuwa na mabadiliko ya muda katika mchezo huo, kwani awali ulikuwa uchezwe saa 10:00 jioni kwa saa za Tanzania ambapo ni saa 11:00 kwa Zambia, lakini umesogezwa mbele na sasa mechi itachezwa saa 12:00 jioni, muda ambao kwa Tanzania ni saa 11:00 jioni.

Stars iliyo Kundi E, ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi tatu sawa na Zambia na Niger, lakini inazidiwa kwa tofauti mabao ya kufunga na kufungwa, huku Morocco ikiongoza kundi kwa pointi sita, baada ya Ijumaa iliyopita kuifunga Zambia mabao 2-1.

Iwapo timu yoyote leo kati ya Stars au Zambia itashinda, itafikisha pointi sita sawa na vinara, Morocco.