Stars kuifuata Zambia kesho

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 11:12 AM Jun 07 2024
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo
Picha: TFF
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo

KIKOSI cha Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), itaondoka nchini kesho kuelekea Zambia kwa ajili ya kucheza mechi ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2026.

Zambia maarufu Chipolopolo itaikaribisha Taifa Stars katika mechi ya Kundi E itakayochezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa ulioko katika Mji wa Ndola.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema jana kikosi cha timu hiyo kimekamilika baada ya nyota ambao walikuwa katika majukumu ya klabu zao kuripoti.

"Kikosi cha Stars sasa kimekamilika, wachezaji wote walioitwa wamewasili, na leo (jana), wamefanya mazoezi kwa Mkapa na kesho (leo), wataendelea kujinoa hapo, wanajiimarisha kwa ajili ya kuhakikisha wanapata matokeo bora huko Zambia," alisema Ndimbo.

Aliongeza benchi la ufundi la Stars lililoko chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Morocco, limesema limeridhishwa na viwango vilivyoonyeshwa na wachezaji katika michezo ya kirafiki iliyofanyika Indonesia wiki iliyopita.

Tanzania inaburuza mkia katika Kundi E ikiwa na pointi tatu sawa na vinara Morocco, Zambia na Niger, hii inatokana na tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa.