Songea United yawa tishio 'Champioship'

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:26 AM Oct 01 2024
TIMU ya Songea United
Picha:Mtandao
TIMU ya Songea United

TIMU ya Songea United, imeanza kuwa tishio kwenye Ligi ya 'Championship', baada ya juzi kushinda mchezo wake wa pili mfululizo, ikiiadhibu Bigman FC, mabao 2-0, katika mchezo uliochezwa, Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, mkoani Ruvuma.

Huu ni ushindi wa pili kwa timu hiyo, katika mchezo wake wa ufunguzi wa ligi hiyo, ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya Kwanza kwenye uwanja huo huo wa nyumbani.

Mabao ya ushindi yalifungwa na nyota wake, Cyprian Kipenye na Ramadhan Kiparamoto.

Kipenye alifunga bao la kwanza dakika ya 66 kwa mkwaju wa penalti, dakika nne baadaye Kiparamoto alipachika bao la pili.

Ushindi huo unaifanya timu hiyo ambayo imebadilishwa jina kutoka FGA Talents iliyokuwa na maskani yake jijini Dodoma, na kuhamia Ruvuma kufikisha pointi sita, huku Bigman, ambayo nayo imebadilishwa jina kutoka Mwadui FC, ikisalia na pointi moja.

Baada ya kukamilika kwa mechi zote nane za raundi ya pili, Mtibwa Sugar inaongoza ikiwa na pointi sita, Songea United nafasi ya pili ikiwa pia na pointi sita, Stand United ya tatu na Biashara United ikiwa nafasi ya nne, zote zikiwa na pointi sita zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Mchezo mwingine juzi uliochezwa, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Mbuni FC ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na wageni, Geita Gold.

Bao la Mbuni lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Emmanuel Julius, lakini Frank Ikobela aliisawazishia, Geita Gold.